Dar es Salaam. Miili ya wanandoa waliokutwa wameuawa chumbani kwao katika eneo la Bonyokwa Gk, Wilayani Ilala jijini Dar es Salaam inatarajiwa kuzikwa katika Kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Vifo vya wanandoa hao Antony (Ally) (46) Ngaboli na Anna (Amina) Amiri (39) vilitokea usiku wa kuamkia Juni 12, 2025 katika makazi yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro jana ilieleza kuwa miili ya wanandoa hao imekutwa ndani ya chumba chao cha kulala huku ikiwa na majeraha na kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendeleaje kujua chanzo cha vifo hivyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 13, 2025 kaka wa marehemu, Rasul Mcharo amesema taratibu za maziko ya marehemu zitaanza baada ya Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi na kukabidhi miili hiyo kwa ndugu.
“Hatuwezi kusema tunazika lini kwa sababu taratibu za uchunguzi zinaendelea na bado kama familia hatujakabidhiwa miili ya marehemu”
“Kama tukikabidhiwa miili ndiyo tutajua tunaaga na kusafirisha lini kwenda kuwapumzisha ndugu zetu kwenye makazi yao ya milele katika Kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro,” amesema kaka wa marehemu.
Amesema marehemu hao watazikwa katika eneo moja kwa kuwa walikuwa wanandoa.
“Kwa mujibu wa mila zetu mwanamke akiolewa anakuwa wa kwetu, hivyo Ally na mkewe watazikwa katika eneo moja,” ameeleza.
Hali ilivyo nyumbani kwa marehemu
Mwananchi imefika katika nyumba ya marehemu hao na kushuhudia watu wakiendelea kufika katika msiba huo huku shughuli mbalimbali za maombolezo zikiendelea huku baadhi ya watu wakiwa katika makundi wakionekana kujadili mambo tofauti.
Mwananchi pia ilishuhudia askari polisi kadhaa ambao walikuwa wakiendelea na uchunguzi.
Mwananchi ilizungumza na msaidizi wa kazi za ndani wa familia hiyo Mariam Said ambaye alieleza alivyogundua tukio hilo jana asubuhi.

Alisema akiwa anafanya usafi nje ya dirisha la wanandoa hao alikutana na hali iliyomtia shaka baada ya kuona dirisha la limevunjwa huku pazia likiwa na madoa mithili ya damu.
“Nilikimbia kumweleza mtoto wao mkubwa ambaye alikimbia kuingia chumbani kwao na kukuta miili ya wazazi wake ikiwa na majeraha, kisha akawapigia simu ndugu waliowashauri kutoa taarifa majirani.
Crédito: Link de origem