top-news-1350×250-leaderboard-1

Mgombea urais apigwa risasi, mtoto atiwa mbaroni

Bogota. Katika hali isiyo ya kawaida  mtoto (15) amekamatwa kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi Seneta wa Colombia anayewania kuwa rais ajaye wa nchi hiyo.

Katika tukio hilo,  seneta Miguel Uribe Turbay (39) akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kampeni yake uliofanyika Bogota nchini humo alijeruhiwa vibaya katika shambulio la mtoto huyo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ya  nchini humo, Seneta huyo alipigwa  jana Jumamosi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika bustani eneo la Fontibon, Mji Mkuu wa Colombia, Bogota.

Ofisi hiyo ilieleza kuwa Turbay alipigwa risasi mbili kutoka nyuma na washambuliaji waliokuwa na silaha kisha kuonekana akitokwa damu kichwani huku akisaidiwa na wasaidizi wake na watu waliokuwa kwenye mkutano huo, kama inavyoonyeshwa kwenye video iliyosambaa mitandaoni.

Kulingana na ripoti ya kitabibu kutoka Hospitali ya Santa Fe Foundation nchini humo, Turbay alilazwa hospitalini humo akiwa katika hali mahututi na bado anafanyiwa upasuaji wa mfumo wa neva na wa mishipa ya damu.

Mkewe, Maria Claudia Tarazone, aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa X kwamba mumewe “anapigania uhai wake” huku akiwahimiza raia wa Colombia kumuombea.

Mashuhuda wa tukio hilo walilieleza Shirika la Habari la Reuters kuwa watu wengine wawili pia walijeruhiwa katika tukio hilo.

Alipoulizwa kuhusu washukiwa wa tukio hilo, Mkuu wa Polisi Jenerali Carlos Triana, alisema mmoja wa washukiwa ambaye ni mtoto mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa), alikamatwa katika eneo la tukio akiwa na silaha na kwa sasa anapatiwa matibabu ya jeraha kwenye mguu.

Serikali imetangaza zawadi ya dola 730,000 (zaidi ya Sh1.9 bilioni) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kutiwa mbaroni mtandao uliohusika kuratibu tukio hilo, huku Rais Gustavo Petro akisema uchunguzi utalenga kubaini ni nani aliyetoa agizo la shambulio hilo.

“Kwa sasa bado ni tetesi tu,” alisema Petro huku akiongeza kuwa kutakuwepo pia uchunguzi kuhusu mapungufu katika ulinzi.

Turbay, ambaye alitangaza nia yake ya kugombea urais kupitia chama cha mrengo wa kulia cha Democratic Center Machi, katika mkutano huo alikuwa ameambatana na timu ya watu 21 wakati wa tukio hilo akiwemo diwani, Andres Barrios.

Alikuwa akitarajia kushiriki kwenye uchaguzi wa urais utakaofanyika Mei 31, 2026 huku akilenga kumrithi Rais Petro, kiongozi wa kwanza wa mrengo wa kushoto nchini humo.

Mama yake, aliyekuwa mwanahabari, alitekwa nyara na kuuawa mwaka 1991 wakati wa moja ya vipindi vya machafuko makubwa zaidi katika historia ya Colombia.

Chama chake kilielezea tukio hilo kama “kitendo kisichokubalika cha ukatili,” huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio akilaani tukio hilo.

Kupitia X, Rubio pia alimshauri rais wa sasa wa Colombia kuwashughulikia maofisa wa ulinzi wa Colombia kwa uzembe ambao umehatarisha maisha ya kiongozi huyo wa kisiasa.
Rais wa zamani wa Colombia, Alvaro Uribe, ambaye hana uhusiano wa damu na Miguel Uribe Turbay, alisema mshambuliaji huyo “amemshambulia kwa risasi mwanasiasa ambaye ni tumaini la nchi, mume mzuri, mwana mzuri, kaka mzuri na mfanyakazi mwenzake wa kipekee.”

Alvaro alighairi safari iliyokuwa imepangwa kwenda Ufaransa kutokana na uzito wa tukio hilo.

Jumuiya ya kimataifa pia imeonyesha kuguswa na tukio hilo ambapo imetoa ujumbe wa mshikamano kutoka kote Amerika ya Kusini, ambapo Rais wa Chile Gabriel Boric alisema: “Hakuna nafasi wala sababu ya ukatili katika demokrasia,” na Rais wa Ecuador Daniel Noboa aliongeza: “Tunakemea aina zote za ukatili na kutovumiliana.”

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.