top-news-1350×250-leaderboard-1

Sababu zatajwa ongezeko watoto njiti Zanzibar

Unguja. Wakati idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya umri (watoto njiti) ikiongezeka Zanzibar, Wizara ya Afya imetaja sababu tano zinazochangia tatizo hilo ikiwa ni pamoja na maambukizi kwa mama ikiwemo ya njia ya mkojo (UTI) na njia ya damu na maambukizi ya maradhi ya kujamiiana (STI).

Sababu nyingine ni afya na lishe duni ya mama au upungufu wadamu, umri mdogo au mkubwa sana wa mama na magonjwa ya kudumu kama vile kisukari au shinikizo la damu.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh amesema takwimu zinaonyesha mwaka 2024, jumla ya wajawazito waliojifungua vituo vya afya na hospitalini walikuwa 52,872 na vizazi hai ni 53,540.

“Kati ya watoto wote waliozaliwa, watoto njiti walikuwa 1,970 (chini ya wiki 37 za ujauzito) sawa na asilimia 3.7,” amesema

Amesema idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 0.6 kutoka mwaka 2023 ambapo watoto waliozaliwa kabla ya wakati walikuwa 1,774 sawa na asilimia 3.1 kati ya jumla ya vizazi hai 57,165.

Akitaja sababu nyingine zinazochangia tatizo hilo, Naibu Waziri Hafidh amesema ni magonjwa yanayohusiana na mimba ikwemo shinikizo la damu wakati wa ujauzito, kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya wakati na ujauzito wa pacha au zaidi.

Pia, tabia na mtindo wa maisha ikwemo kufanya kazi nzito sana na msongo wa mawazo au ukatili wa kijinsia na kuchelewa kufika vituoni kwa wakati ili kupata huduma stahiki pale changamoto zinapojitokeza.

Awali mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir alitaka kujua tathmini ya mama wajawazito wanaojifungua watoto njiti ikoje kwa sasa.

Naye Mwakilishi wa Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman amesema katika vituo vya afya vinakabiliwa na changamoto ya washauri nasihi akitaja kuwa wazazi wanakosa kupata ushauri mzuri ili kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo akihoji mpango wa serikali wa kuongeza wahudumu.

Naibu Waziri Hafidh amekiri sekta hiyo nzima kukabiliwa na uhaba wa wataalamu lakini akataja mpango wa serikali ni kuendelea kuongeza wataalamu hao na kwamba inazidi kutoa elimu kwa wananchi kwani kazi yake ya kwanza kabla ya kutibu ni kukinga

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.