Dodoma. Katika Bunge la wiki hii, wizara nne zinatarajiwa kuingia kwenye mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26, huku baadhi ya wananchi wakitaka Serikali kutoa majibu ya haraka kuhusu matukio ya watu waliotekwa, kupotea au kuuawa.
Wizara hizo ni pamoja na ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Hoja kuu zinazotarajiwa kuibuka wakati wa mjadala huu ni pamoja na changamoto za kuvunjika kwa ndoa, suala la uraia pacha na migogoro ya ardhi.
Kesho, Mei 26, 2025, Wizara ya Mambo ya Ndani itakuwa ya kwanza kuwasilisha bajeti yake. Moja ya changamoto kubwa inayokabili wizara hii ni utekaji unaofanywa na watu wasiojulikana.
Baadhi ya wanaodaiwa kutekwa au kuchukuliwa na watu wasiojulikana na mpaka sasa hawajulikani walipo ni pamoja na Deusdedith Soka, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Temeke, Katibu wake Jacob Mlay na Ally Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, ambaye alichukuliwa akiwa ndani ya basi la Tashrif Tegeta jijini Dar es Salaam na baadaye kupatikana amefariki dunia.
Mwingine ambaye hajulikani alipo ni mwanaharakati Mdude Nyagali, aliyechukuliwa nyumbani kwake. Jeshi la Polisi limeahidi linafanyia kazi suala hilo.
Kilio cha kutaka hatua zichukuliwe hakijatoka tu kwa vyama vya siasa na ndugu wa waathirika, bali pia taasisi binafsi kama Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na viongozi wa dini, wakitaka Serikali ichukue hatua madhubuti kukomesha utekaji, upoteaji na mauaji hayo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 25, 2025, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema changamoto hiyo ni ya kimfumo, na kuiongezea bajeti Wizara ya Mambo ya Ndani, haitaweza kutatua tatizo hilo kama mifumo haitaimarishwa.
“Kuna mambo ya muda mfupi na mrefu, mafunzo ya polisi yanahitaji kuboreshwa, wawe na elimu ya kutosha na wafundishwe kuheshimu haki za binadamu. Pia tunapaswa kubadilisha jina kutoka Jeshi la Polisi kuwa huduma ya usalama wa raia ili kubadilisha mtazamo,” amesema.
Ameongeza kuwa mfumo mzima wa polisi unapaswa kufumuliwa, masilahi yao kuboreshwa na vifaa vya kazi kuimarishwa.
Amesema kwa hatua za haraka anazofikiri zitaweza kusaidia kutatua changamoto hiyo, Serikali inapaswa kutoa majibu kwa haraka juu ya matukio yote ya utekaji, upoteaji na mauaji yanayolalamikiwa na wananchi, pamoja na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.
Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa chombo maalumu kitakachosimamia na kufuatilia matukio yote yanayohusu vyombo vya usalama, kikisimamiwa moja kwa moja na Rais mwenyewe.
Kwa mwaka 2024/25, Wizara ya Mambo ya Ndani iliidhinishiwa bajeti ya Sh1.71 trilioni, Sh289.69 bilioni zilitengwa kwa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa changamoto za maadili na ndoa za jinsia moja kwa mwaka uliopita, wabunge waliikosoa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushindwa kuonyesha mikakati ya kupambana na ndoa hizo na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na vijana.
Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Katiba na Sheria waliingilia kati wakieleza hatua walizochukua, ikiwemo kuwatimua wakimbizi waliobainika kujihusisha na ndoa hizo.
Mwanaharakati wa masuala ya jinsia, Janeth Mawinza akizungumzia hilo, amesema mmomonyoko wa maadili unasababishwa kwa kiasi kikubwa na wazazi au walezi kushindwa kuzungumza na watoto wao.
“Serikali iwaelimishe wazazi kuhusu umuhimu wa kuzungumza na watoto. Watoto wanajifunza kwa kuona na kusikia, hivyo kukosa muda wa mazungumzo kunawaweka hatarini,” amesema Janeth, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI).
Kwa mwaka 2024/25, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ilitengewa jumla ya Sh67.90 bilioni huku Sh20.41 bilioni zikitengwa kwa miradi ya maendeleo.
Licha ya jitihada mbalimbali za Serikali, migogoro ya ardhi inaendelea kuwa changamoto kubwa nchini.
Serikali iliunda timu ya mawaziri wanane waliotembelea maeneo mbalimbali ili kutatua migogoro hiyo, ikiwa ni pamoja na mawaziri wa Tamisemi, kilimo, mifugo, uvuvi, mazingira, maliasili na utalii, ulinzi na maji.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Dk Angelina Mabula, aliwahi kueleza kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni pamoja na kumilikisha watu zaidi ya mmoja kiwanja kimoja, pamoja na changamoto za ulipaji fidia. Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma imetajwa kuathirika zaidi.
Mei 23, 2025, Waziri wa Ardhi, Deogratius Ndejembi alisema Serikali iko mbioni kuanzisha Tume ya Taifa ya Ardhi (Land Commission) kama suluhisho la kudumu.
Mkazi wa Miyuji, Dodoma, Gaspar Masawe, amesema migogoro hii inahitaji uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha watumishi wa ardhi wanakuwa waadilifu.
Mwaka 2024/25, Wizara ya Ardhi iliidhinishiwa bajeti ya Sh171.37 bilioni, ambapo Sh75.69 bilioni zilienda katika miradi ya maendeleo.
Suala la uraia pacha
Kwa muda mrefu, Watanzania wenye uraia wa nchi mbili wamekuwa wakipigania kutambuliwa rasmi kupitia uraia pacha. Serikali iliwasilisha muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Uhamiaji na Sheria ya Ardhi, ili kuweka utaratibu wa hadhi maalumu.
Hata hivyo, Novemba 8, 2024, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alitangaza kuondolewa kwa muswada huo bungeni kwa mara ya pili, baada ya kuondolewa pia Septemba 4, 2024. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya kuifanyia kazi zaidi hoja hiyo.
Suala la uraia pacha linatarajiwa kuibuka tena kwenye mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo kwa mwaka wa fedha 2024/25, iliidhinishiwa Sh241.06 bilioni, ambapo Sh11.63 bilioni zilitengwa kwa miradi ya maendeleo.
Crédito: Link de origem