Dar es Salaam. Ofisa Afya mstaafu wa Wilaya ya Bagamoyo, Farah Abdi amesimulia namna alivyoupokea mwili wa binti anayedaiwa kuuawa kwa kisu na mama yake mzazi akishirikiana na kaka yake, kwa ajili ya kuuhifadhi kabla ya kuuzika kisha ukafukuliwa kwa uchunguzi.
Abdi ametoa simulizi hiyo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na Hakimu Mkazi aliyepewa mamlaka ya ziada, Mary Mrio.
Shahidi wa nane katika kesi ya mauaji ya kifamilia ambapo mama anadaiwa kumuua binti yake akishirikiana na kijana wake wa kiume, amesimulia namna alivyopokea mwili wa marehemu (mwanafamilia huyo) kutoka kwa askari Polisi kuuhifadhi baada ya kuokotwa kichakani, na jinsi ulivyozikwa na kisha kufukuliwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sophia Mwenda na mtoto wake wa kiume, Alphonce Magombola.
Wote wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafamilia, Beatrice Magombola, wakidaiwa kutenda kosa hilo Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa upande wa maelezo ya upande wa mashtaka, katika kutekeleza tukio hilo, Alphonce alimfunga miguu dada yake Beatrice na kumshikilia mikono kisha mama yake, Sophia, akamchomachoma bintiye yake huyo kwa kisu kwenye titi la kushoto mpaka alipofariki dunia.
Wanadaiwa kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo walikwenda kuutupa mwili kichakani eneo la Zinga, wilayani Bagamoyo.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliamua kutekeleza mauaji hayo kwa kuwa mwanafamilia huyo alitaka kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao.
Katika ushahidi wake, jana, Mei 20, 2025, Abdi ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mashtaka ameieleza Mahakama hiyo kuwa wakati wa tukio hilo yeye ndiye alikuwa ofisa afya wa Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa ushahidi wake alioutoa akiongozwa na Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilinge, Desemba 2, 2020 akiwa ofisi kwake katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, walifika askari Polisi
Kutoka kituo cha Polisi Bagamoyo wakiwa na mwili wa mtu wa jinsia ya kike.
Askari hao walimweleza Abdi kuwa wameuokota mwili huo eneo la Zinga na wakataka ufanyiwe uchunguzi wa kitabibu kujua chanzo cha kifo cha mtu huyo.
Mwili huo ulikuwa na jeraha la kuchanwa na kitu chenye ncha kali chini ya titi la kushoto na usoni na baada ya kufanyiwa uchunguzi huo, kwa kuwa ulikuwa haufahamiki waliuhifadhi mochwari kusubiri kama utatambuliwa.
Hata hivyo mpaka Machi 16, 2021, ulikuwa bado haujatambuliwa, hivyo walifanya mawasiliano na Polisi Bagamoyo kuhusu gharama za kuendelea kuuhifadhi.
Polisi walitoa idhini, wakauzika katika makaburi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, kazi iliyofanywa na timu iliyomuhusisha Mkuu wa mochwari, na watumishi wengine wa Hospitali ya Wilaya walioajiriwa kwa kazi hizo, chini ya usimamizi wake Abdi.
Aprili 5, 2022 walifika askari kutoka Oysterbay Dar es Salaam, wakamueleza kuwa wanafuatilia mwili huo, huku wakionesha kibali cha Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo cha kufukua maiti hiyo.
Kaburi lilikuwa na alama ya utambulisho kama inavyofanyika kwa miili yote isiyotambulika inapozikwa na halmashauri, ambazo ni pamoja na tarehe na mahali mwili ulikookotwa na jinsia.
Mwili ule ulifukuliwa mbele ya katibu wa Kitongoji cha Ufundi na wananchi wengine ambao walikuwa ameshaanza kusogea na ulikutwa tayari umeshaanza kuharibika kwa kumomonyoka nyama sehemu mbalimbali.
Polisi baada ya kuufukua walichukua sampuli kisha ukarejeshwa kaburini.
Wakati wa maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili wa utetezi, Hilda Mushi, shahidi huyo alieleza kuwa wanapopokea mwili wanausajili katika rejista ya mochwari, lakini hakuitoa mahakamani rejista hiyo.
Amesema kuwa wanaweza kukaa na mwili usiojulikana mpaka aliyeupeleka atakapotoa idhini ya kuuzika na hakuna muda maalumu wa kukaa nao, kwani wanaweza kukaa nao hata kwa miaka mitatu.
Shahidi huyo amekiri kuwa hakuieleza mahakama kuwa walipata wapi kibali cha kwenda kuzika mwili huo katika makaburi hayo ya halmashauri.
Amesema kuwa walikwenda kuuzika kwa idhini ya askari aliyeupeleka, baada ya kumuandikia barua Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), huku akikiri kuwa hata hiyo barua hajaitoa mahakamani kuithibitishia Mahakama.
Vilevile amekiri kuwa hawakuwahi kutangaza kuwa kuna mwili uliookotwa.
Ingawa amesema kuwa askari Polisi walichukua sampuli lakini amekiri kuwa hakuona ni kitu gani hasa askari wale walichukua katika mwili ule.
Vilevile amekiri kuwa siku hiyo ya Machi 16, 2021 walizika miili zaidi ya mmoja lakini akakana kuzika baadhi ya miili katika kaburi moja akisisitiza kuwa kila mwili ulizikwa pekee yake.
Akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili Godwin Fisoo, shahidi huyo ameeleza kuwa Mahakama ilitoa kibali cha kufukua mwili wa Baatrice Magombela, kama walivyoelezwa na Polisi katika maelezo ya awali ya polisi.
Kesi hiyo bado inaendelea kwa shahidi wa tisa.
Crédito: Link de origem