top-news-1350×250-leaderboard-1

Shahidi aeleza alivyogundua mwili kichakani mauaji ya kifamilia

Dar es Salaam. Shahidi wa sita katika kesi ya mauaji ya kifamilia inayomkabili mama anayedaiwa kumuua binti yake akishirikiana na kijana wake wa kiume, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, namna alivyobaini mwili wa marehemu uliokuwa umetupwa kichakani.

Washtakiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, mwenye mamlaka ya ziada, Mary Mrio ni Sophia Mwenda na mtoto wake wa kiume, Alphonce Magombola.

Wote wanaokabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafamilia, Beatrice Magombola, wakidaiwa kutenda kosa hilo Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa upande wa maelezo ya upande wa mashitaka, katika kutekeleza tukio hilo, Alphonce alimfunga miguu dada yake Beatrice na kumshikilia mikono kisha mama yake, Sophia, akamchomachoma bintiye yake huyo  kwa kisu kwenye titi la kushoto mpaka alipofariki dunia.

Wanadaiwa kuwa waliamua kutekeleza mauaji hayo  kwa kuwa mwanafamilia huyo alitaka kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao. 

Katika ushahidi wake jana, Mei 19, 2025 shahidi wa sita upande wa mashitaka katika kesi hiyo ,Godfrey Elisha, mkazi wa Zinga Bagamoyo, ameieleza Mahakama kuwa ndiye aliyeuona mwili wa Beatrice na kutoa taarifa Polisi.

Akiongozwa na mwendesha mashitaka, wakili wa Serikali Pauline David, shahidi huyo anayefanya kazi ya ulinzi, ameieleza Mahakama kuwa siku hiyo Desemba 2, 2020  saa 11:30 asubuhi, akiwa anakwenda kazini eneo la Zinga  Viwandani, aliona furushi kubwa kichakani.

Kwa mujibu wake shahidi huyo, furushi hilo lilikuwa limezungushwa mkeka na kufungwa kwa shuka, ambapo alipolisogelea na kuangalia vizuri aliona mkono umetokeza nje ya furushi, lakini  hakutambua jinsia yake.

Katika eneo hilo pia kulikuwa na ndoo ndogo nyeupe yenye mfuniko wa bluu ambapo ndani kulikuwa na nguo zilizokuwa na damu na viatu.

Hivyo alimpigia simu Mwenyekiti wa kijiji cha Zinga, Hamisi Magulumbasi, kumweleza tukio hilo pamoja na askari wa Kituo cha Polisi Bagamoyo aliyemtaja kwa jina la Inspekta Gerald, ambaye alifika na askari wenzake  Philipo na Yohana wakiwa na gari.

Wakati askari hao wanafika na gari hilo tayari kulikuwa kumeshapambazuka na wananchi walikuwa wameshaanza kusogea.

Askari hao walisogelea furushi hilo , wakafungua na kugundua mkono wa mwanamke ambaye alikuwa amesuka, akiwa amevaa blauzi nyeusi na taiti nyeupe, huku kwenye ziwa la kushoto na mdomoni mwili huo ukiwa na majeraha.

Askari hao walipiga picha eneo hilo kisha waliondoka na mwili naye Elisha alikwenda kuomba ruhusa kazini ili kwenda kuandika  maelezo Kituo cha Polisi Bagamoyo kuhusu tukio hilo, kile alichokiona.

Machi 29, 2022, Elisha alipigiwa simu na Mwenyekiti, Magulumbasi akimtaka aende ofisini kwake anahitajika na askari kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Askari hao walimuhoji, naye aliwaeleza alichokiona siku ya  Desemba 2 ,2020.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi wengine wa Jamhuri,  Machi 16, 2021 saa nne asubuhi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhani Kingai  kwa sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kupotea kwa Beatrice Magombola.

Msiri huyo alidai kuwa kumekuwa na taarifa za utata kuhusu kupotea kwake kwani mama mzazi wa Beatrice, Sophia (mshtakiwa wa pili), anadai kuwa mtoto wake amekwenda Afrika Kusini, kwa ajili ya matibabu na wakati mwingine akiulizwa anadai amekwenda Canada kutibiwa.

Alidai kuwa hata hivyo mama huyo alikuwa haweki wazi ugonjwa unaomsumbua Beatrice na taarifa kuhusu hali hiyo hazikuwa zikifahamika kwa ndugu wa Beatrice wala baba yake mzazi, isipokuwa kaka yake mkubwa Alphonce, mshtakiwa wa kwanza.

Msiri huyo alieleza kuwa, Beatrice alikuwa na gari aina ya Vanguard lililokuwa likitumiwa na Alphonce na pia nyumba yake iliuzwa na Sophia na kuna wakati washtakiwa hao wakihojiwa kupotea kwa Beatrice wanakuwa wakali.

Kutokana na taarifa hizo za msiri, Kamanda Kingai alielekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi na upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kukamatwa kwa washtakiwa hao.

Washtakiwa katika maelezo yao ya onyo wanadaiwa kuwa walikiri kumuua Beatrice na kufunga mwili wake kwa shuka na mkeka wa Kichina na kwenda kuutupa eneo la Zinga, Bagamoyo.

Walieleza kuwa walimuua Beatrice kwa sababu alikuwa anataka kwenda kutoa ushahidi mahakamani Mbeya katika kesi ya nyumba ya familia ambayo wao (washtakiwa) waliiuza.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa shitaka hilo Julai 15, 2022.

Kesi hiyo inaendelea leo Mei 20, 2025 kwa mashahidi wengine wa Jamhuri.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.