Bukoba. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kukiamuru Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuitisha upya Baraza kuu ili kuziba nafasi ya wajumbe wanane, chama hicho kisitafute mchawi bali wao ndio wenye makosa.
Kauli hiyo ya CCM, imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Amos Makalla aliyelitaka Chadema kutopeleka shutuma kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa sababu ofisi hiyo imeteleleza majukumu yake.
Mei 12, 2025 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilikiandikia barua Chadema ikikitaka kuitisha upya baraza kuu, uamuzi ambao dhahiri umetengua uteuzi wa wajumbe wanane wa kamati kuu na sekretarieti waliothibitishwa katika kikao cha baraza kuu kilichoketi Januari 22, 2025.
Hatua hiyo ya Msajili imefanyika ikiwa ni kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na kada wa Chadema, Lembrus Mchome akipinga akidi ya baraza kuu iliyowathibitisha.
Mchome alikuwa akilalamikia akidi kuwa haikutimia ya kuwathibitisha viongozi hao ambao walikuwa wameteuliwa na Mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu.
Hivyo, kutokana na hilo, uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa aloutoa ni wa kuwaweka kando mpaka Baraza kuu jingine litakapoitishwa, ni pamoja na Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Pia, aliwataja wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na Baraza Kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ambaye pia aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Hata hivyo, kupitia mikutano yake ya hadhara aliyoifanya katika maeneo mbalimbali nchini, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesisitiza hakuna watakachokibadilisha ili kutii maelekezo ya Msajili huku akisema bado wanawatambua Mnyika na wenzake kama viongozi halali wa chama hicho.
Leo Jumapili Mei 18, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kashai wilayani Bukoba mkoani Kagera, Makalla amesema; “wao (Chadema) wenyewe ndio wametuhumiana, mara akidi haijakaa sawa, Mchome ( Lembrus kada wa Chadema) kabeba kaipeleka kwa Msajili. Haya leteni ushahidi wa akidi hawana muhtasari, badala yake wanatafuta mchawi.
“Wanatafuta mchawi wawapi? miongoni mwenu ndio mmekwenda kushtakiana kwa msajili, wasitafute mchawi Chadema wanaiua kwa mikono yao wenyewe, CCM ingependa kuwa na upinzani… lakini inshallah wameamua wenyewe,” amesema Makalla.
Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema, Dk Nshala Rugemeleza amesema maelezo ya mwenezi wa CCM ni propaganda za kisiasa.
Amesema Makalla anaufahamu ukweli wote kuhusiana na sakata hilo.
“Chadema tunaendelea kusisitiza yote yaliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, yapo kinyume cha sheria na ushahidi upo wazi, kuna kampeni zinaendelea lakini mwisho wa siku kila kitu kitakuwa wazi,” amesema Dk Rugemeleza.
Katika ziara hiyo, Makalla amewataka wananchi wa Kagera kukataa wanasiasa wanaoeneza chuki na mgawanyiko, akisisitiza uchaguzi mkuu utafanyika kama ulivyopangwa na Serikali.
Mbali na hilo, Makalla amesema mkoa huo umepiga hatua mbalimbali za maendeleo kuanzia sekta za miundombinu, afya na elimu huku akiwashangaa wanaosema Kagera kuna umasikini, amewataka kuwapuuza watu hao.
“Wanasema kuna umasikini, baada ya mkutano wao wanaendesha ‘tone tone’ (harambee ya kuchangia fedha kutoka kwa wananchi), hawa hawa waliosema masikini…,” amesema Makalla.
Naye Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rwekiza amesema jimbo hilo lipo tayari kwa uchaguzi, hawadanganyiki na ajenda ya No reforms no election kwa sababu Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sh126.6 bilioni.
Mbunge mwingine wa Bukoba Mjini, Steven Byabato amesema kazi kubwa imefanywa na Serikali na katu hawatamuangusha Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“CCM haitafanya makosa yaliyofanyika huko wa jimbo hili kuchukuliwa na upinzani, sasa hivi ni CCM mbele kwa mbele,” amesema Byabato.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa kimkakati wa barabara ya njia ya nne eneo la Bukoba mjini akisema ukikamilika utarahisisha uboreshaji wa miundombinu.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema mkoa unaendelea kupiga hatua za maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, miundombinu na afya ili kuboresha huduma za jamii mkoani humo.
Crédito: Link de origem