Dar es Salaam. Mwakilishi wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi ametumia dakika 20 kunadi sera zake akijikita kwenye maeneo makuu manne, huku akitaja vipaumbele vyake saba.
Profesa Janabi amenadi sera hizo leo Jumapili, Mei 18, 2025 mbele ya Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kanda ya Afrika katika kikao cha ana kwa ana kinachoendelea jijini Geneva, Uswisi kwa ajili ya kumchagua mkuu wa kanda ajaye.
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo Mtanzania Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti 27, 2024, aliyefariki dunia Novemba 27, 2025 wakati akipatiwa matibabu nchini India.
Kupitia jukwaa hilo, Profesa Janabi alianza kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpendekeza.
Pia ametoa pole za dhati kwa kumpoteza Dk Faustine Ndugulile hali iliyochangia kurudiwa kwa uchaguzi huo, kisha alijitambulisha maeneo manne atakayoyagusia ikiwemo wasifu wake, mchango wake, maono na mikakati.
Ameelezea miaka 30 ya kufanya kazi ya afya ya umma na kuelezea alianza kufanya kazi kama mtafiti.

“Safari yangu ilianza kwa unyenyekevu nikiwa daktari mchanga, na kupitia miaka ya kazi kwa bidii, kujitolea, uwajibikaji na uongozi, nilipanda hadi kufikia cheo cha Profesa wa magonjwa ya moyo na msimamizi wa afya.
“Zaidi ya kazi yangu ya kitabibu, nimetumikia kama ofisa wa hesabu, mtaalamu wa afya ya umma, mtafiti, mwanasayansi, mwandishi, mwanaakademia, na balozi wa afya, nikipata uelewa wa kina kuhusu changamoto tata za kiafya duniani, ikiwemo katika mazingira ya migogoro.”
Profesa Janabi ameeleza miaka 10 aliyofanya kazi kama daktari na mashauri wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tangu mwaka 2005 mpaka 2015.
Amesema miaka ya 2000, alishiriki katika tafiti za majaribio ya VVU kati ya Tanzania na Msumbiji.
Kazi yake mwaka 2012 ilisababisha Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, kufanyiwa vipimo vya VVU hadharani, hatua iliyosaidia kuondoa unyanyapaa na kuwahamasisha Watanzania milioni tano kupima na kupata ushauri nasaha.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena mwaka 2021, Rais Samia alipojitokeza hadharani kuhimiza chanjo ya Covid-19, hatua iliyoongeza kwa kiasi kikubwa uchanjaji na kupunguza upotoshaji wa taarifa.
Amesema amefanya kazi katika maeneo mengi na baadaye Rais Samia alimwamini na kumfanya kuwa mshauri wake wa masuala ya Afrika na namna alivyoshiriki katika kutokomeza ugonjwa wa Marburg mwaka 2023 na 2025.
Akitaja uzoefu na mafanikio yake binafsi, Profesa Janabi amesema kuwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alipunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95, hatua iliyoiwezesha Tanzania kuokoa zaidi ya dola milioni 10 kwa mwaka.
Fedha hizo, amesema, zilielekezwa kwenye kuimarisha huduma za Afya ya Msingi (PHC), hivyo kunufaisha watu waliokuwa hawawezi kumudu matibabu ya hospitalini.
Amesema hayo, yalifanikishwa kupitia kujenga uwezo wa ndani wa wataalamu, kuboresha miundombinu, kutetea ongezeko la bajeti ya afya, kushirikiana na sekta binafsi na kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Amesema JKCI sasa imekuwa kituo cha kikanda kinachofanya zaidi ya upasuaji wa moyo wazi na taratibu za tiba ya moyo kwa wagonjwa 4,000 kwa mwaka, ikiwemo upandikizaji wa betri za moyo na upasuaji ikiwanufaisha wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.

Mwaka 2022, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), moja ya hospitali kubwa zaidi katika kanda hiyo, ikiwa na vitanda zaidi ya 2,400 na wafanyakazi zaidi ya 4,000. Hospitali hiyo inahudumia wastani wa wagonjwa 3,800 kwa siku.
“Zaidi ya hayo, ninasimamia mtandao wa vituo vidogo vya afya 12,200 kote nchini kupitia tiba mtandao, tiba-elektroniki na akili bandia. “Mpango wetu ni kuwafundisha wahudumu wa afya wa jamii 137,000 ifikapo 2030 ili kuwa kiungo kati ya jamii na mfumo rasmi wa afya,” amesema.
Chini ya uongozi wake, Profesa Janabi amesema Muhimbili ilipata ufadhili wa dola milioni 363 za Marekani, mwaka 2025 kutoka kwa mfadhili mpya, Jamhuri ya Korea Kusini, kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa afya.
Fedha hizo amesema, zilitolewa kwa masharti nafuu, zikiwa na riba ya asilimia 0.01, kipindi cha neema cha miaka 15 na muda wa kulipa wa miaka 25.
“Ufadhili huu wa kibunifu utageuza Muhimbili na vituo vyake vya afya kuwa kitovu cha kikanda cha huduma za kinga, tiba, ulinzi na urejeshaji wa afya,” amesema.
Akiwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, ameahidi kushirikiana na wafadhili wa aina hiyo kutoka Afrika na kwingineko.
Akitaja vipaumbele vyake, Profesa Janabi amesema atahakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC) unaoendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akibainisha kuwa Afrika imechelewa katika utekelezaji wake.
Kipaumbele cha pili ni ufadhili endelevu, ambapo ameeleza kuwa nchi wanachama huchangia asilimia 20 pekee ya bajeti ya WHO.
Hali hiyo, amesema, inazuia uhuru wa shirika hilo, hivyo anaunga mkono kuongeza michango ya lazima na kupanua vyanzo vya fedha kupitia bima ya afya, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, uwekezaji mseto, ubadilishaji wa madeni kwa afya, na kufutwa kwa madeni ya kimataifa.
Kipaumbele cha tatu ni maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, ambacho kinajumuisha kuimarisha nguvu kazi ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha mifumo ya mwitikio wa haraka, na kukuza ushirikiano wa mipakani.
Katika afya ya mama, mtoto na lishe, amesema Afrika inachangia asilimia 70 ya vifo vya wajawazito na asilimia 56 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani.
Hata hivyo, Tanzania ilipunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80 kati ya 2015 na 2022, mafanikio yaliyotambuliwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipokea tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates mwaka 2024.
Profesa Janabi pia ameahidi kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na magonjwa yaliyopuuzwa kwa kutekeleza mikakati thabiti ya kudhibiti magonjwa, kukuza maisha yenye afya, na kutambua uhusiano kati ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.
Kipaumbele cha sita ni kupambana na usugu wa vimelea vya dawa (AMR), tatizo linalosababisha vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku asilimia 40 ya mataifa ya Afrika yakikosa takwimu za ufuatiliaji. Ameahidi kuanzisha hifadhidata za kikanda kukabiliana na tatizo hilo.
Kipaumbele cha saba ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya, ikiwemo chanjo, dawa na pia alisema ataboresha tafiti.
Amesema janga la Covid-19 lilidhihirisha utegemezi mkubwa wa Afrika kwa uagizaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba, ambapo zaidi ya asilimia 99 ya bidhaa hizo zilikuwa zinatoka nje.
“Nitatumia diplomasia ya afya kuimarisha ushirikiano wa mifumo ya afya na kuinua uongozi wa Afrika katika afya ya kimataifa,” amesema.
Katika kipindi cha maswali na majibu, Profesa Janabi aliulizwa maswali kadhaa yaliyojikita katika sera zake na namna atakavyotekeleza, huku mengine yakiwa nje ya sera zake.
Akijibu maswali hayo, amesema ataangalia changamoto zilizopo na namna atakavyozifanyia kazi, huku akisisitiza namna ambavyo watoa huduma ngazi ya jamii wana nafasi kubwa ya kuokoa maisha iwapo watatumika ipasavyo.
“Watoa huduma ngazi ya jamii wamejenga imani kwao, tukiwaweka hawa mbele na kuwapa elimu kuhusu chanjo, afya ya umma na afya ya mama wajawazito.”
Akijibu swali kuhusu afya kwa wote amesema changamoto katika nchi nyingi wanaojiunga na mifuko ya bima asilimia 80 yao tayari wanaumwa na asilimia 20 ni wazima, hivyo bima haiwezi kufanya kazi lazima asilimia kubwa wawe si wagonjwa, hivyo bima ya afya kwa wote kiwe kipaumbele kwa kila nchi ili wasio na fedha mfukoni wapate matibabu wakiugua.
Alipoulizwa swali jingine kutoka Morocco, kuhusu namna atakavyokabiliana na athari za magonjwa ya mlipuko, ikiwemo chanjo kwa watoto amesema ni suala ambalo atalishughulikia baada ya kukaa na sekretarieti na kuona namna ya kuyafanyia kazi.
Gambia iliuliza swali kuhusu changamoto ya upatikanaji wa dawa nzuri na namna ya changamoto ya ufikishwaji wa dawa katika maeneo yasiyofikika.

Profesa Janabi amesema dawa ni ghali na hali ya uchumi wa nchi nyingi za Afrika hazimudu, hivyo watakuja na mikakati ya makubaliano na wenye viwanda vya uzalishaji chanjo akiitaja GAVI na Global Fund.
“Afrika ni wakati mzuri wa kuwa na viwanda vyetu, tuna nafasi nzuri tunaweza kutengeneza watu wetu na tukawa na viwanda vyetu tukazalisha dawa na vifaatiba, tunaweza kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa zipo nchi nyingi kama Misri, Afrika Kusini,” amesema.
Crédito: Link de origem