Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limepunguza nusu ya timu yake ya usimamizi na italazimika kupunguza shughuli zake baada ya Marekani kutangaza inaondoka katika shirika hilo na kusitisha ufadhili.
Pamoja na uamuzi huo, WHO inakusudia kufunga baadhi ya ofisi zake katika nchi zenye kipato cha juu.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano, Mei 14, 2025 na Shirika la Habari la Reuters, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema hayo katika kikao cha kamati ya bajeti kabla ya mkutano wa mwaka wa shirika hilo wiki ijayo.
“Kwa kusema wazi, hatuwezi kufanya kila kitu,” amesema Dk Tedros.
Januari 20, 2025, Rais wa Marekani, Donald Trump wa Marekani alisema nchi yake inaondoka katika shirika hilo, ambapo ilikuwa ni siku ya kwanza tangu kurejea kwa mara nyingine madarakani.
Kulingana na sheria ya Marekani, kipindi cha notisi ya mwaka mmoja kinahitajika kabla ya nchi hiyo kujitoa, ambayo ni mfadhili mkubwa zaidi wa WHO, pamoja na kulipa ada zote. Hata hivyo fedha hizo bado hazijalipwa.
Dk Tedros amesema shirika hilo pamoja na nchi wanachama wake lazima wachague kwa uangalifu vipaumbele vyao, kufuatia pendekezo la kupunguza bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa asilimia 21 hadi dola bilioni 4.2.
Hata bajeti hiyo iliyopunguzwa itakuwa imefadhiliwa kwa karibu asilimia 60, iwapo nchi wanachama zitakubaliana kuongeza ada zao za lazima kwenye mkutano ujao, amesema.
WHO tayari imetangaza hatua za kuboresha ufanisi na inatarajia kuokoa takriban Dola 165 milioni mwaka huu.
Pia, itapunguza idadi ya idara zake kutoka 76 hadi 34 na inapanga kupunguza gharama za wafanyakazi kwa asilimia 25.
“Kupunguza ukubwa wa wafanyakazi wetu kunamaanisha kupunguza ukubwa na wigo wa kazi yetu,” amesema.
Dk Tedros amesema WHO imefanya mazungumzo na mashirika mengine ya afya duniani, kujadili ushirikiano zaidi kutokana na kupunguzwa bajeti.
Timu mpya ya uongozi ya shirika hilo sasa ina watu saba, akiwemo Dk Tedros, kutoka idadi ya awali ya watu 14.
Mabadiliko hayo yanajumuisha kumhamisha Mwanasayansi Mkuu Dk Jeremy Farrar hadi nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa Uendelezaji wa Afya na Kinga.
Dk Chikwe Ihekweazu atakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya Dharura za Kiafya, na Dk Sylvie Briand atakuwa Mwanasayansi Mkuu.
Crédito: Link de origem