Guangzhou, China. Wakati Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, taasisi zake nazo zinatoa ushirikiano kwa sekta binafsi baada ya ubalozi mdogo mjini Guangzhou nchini China pamoja na ofisi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuwapokea wateja 36 wa Benki ya CRDB waliokwenda kushiriki Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Canton yanayoendelea nchini humo.
Wawakilishi hao wa Serikali nchini China wamewapokea wafanyabiashara hao baada ya siku kadhaa za kutembelea masoko na viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali ambazo zinahitajika nchini.
Akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandalia mahsusi kwa ajili ya ujumbe huo wa wafanyabiashara, Balozi Mdogo wa Tanzania nchini China, Khatibu Makenga amepongeza hatua ya benki hiyo kwa wateja wake akisema ziara kama hizo husaidia kufungua fursa ambazo zisingeonekana kirahisi iwapo mfanyabiashara angekuwa amejifungia nyumbani.
“Ziara hizi huwa naziita za kujifunza kwa sababu mliopata bahati hii naamini hamtorudi bure. Mmejifunza kuhusu huduma kwa wateja, mmeanzisha uhusiano na viwanda na mmeona mambo yatakayowasaidia kuimarisha biashara zenu. Mnaporudi nyumbani, nendeni mkajitofautishe na wengine ili nao waige kutoka kwenu,” amesema Balozi Makenga.
Pia Balozi Makenga amewakumbusha wafanyabiashara hao kutoa mrejesho wa huduma wanazozipata kutoka CRDB na maeneo mengine kwani, kwa kufanya hivyo huzisaidia taasisi husika kuona umuhimu wa kile wanachokifanya hivyo kuongeza ubunifu na kutanua wigo ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
“Kwenye biashara jambo muhimu ni kukua, mkirudi nyumbani ukaboresha biashara yako, utakua. Kipato chako kitaongezeka na kadri biashara yako itakavyokua ni vizuri kuwataja waliochangia.
Ukiwaambia CRDB kwamba ziara mliyonipeleka China ilinisaidia kwa namna hii au mkopo mlionipa uliniinua kwa kiasi hiki utawashawishi wengine kutambua umuhimu wa huduma za benki. Watakufanya wewe kuwa mfano wao wa kuigwa na watazitumia huduma za taasisi zetu kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla,” amesisitiza Balozi Makenga.

Akiwakaribisha wafanyabiashara hao kutumia huduma za ndege, Mwakilishi Mkuu wa ATCL nchini China, Josephat Kagirwa amesema ni jambo la kujivunia kwa Serikali kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Guangzhou kwani ni nchi chache Afrika zenye safari za moja kwa moja kwenda China.
“Tulianza safaari za kuja China mwaka 2022 tukiwa na mruko mmoja tu kwa wiki lakini sasa hivi ni mara tatu kwa wiki. Tunapokea mizigo mingi hadi tunakosa pa kuiweka.
Tunasafirisha kati ya tani 15 paka 20 sasa hivi kutegemea na idadi ya abiria wanaosafiri siku hiyo. Zamani, idadi ya Watanzania ndani ya ndege ilikuwa ndogo lakini sasa imeongezeka,” amesema Kagirwa.
Mwakilishi huyo wa ATCL aliwasisitiza wafanyabiashara hao kuangalia fursa za kusafirisha bidhaa kutoka Tanzania kwenda China akisema eneo hilo bado Tanzania haifanyi vizuri licha ya uwezekano wa kuwanufaisha wengi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwakala wa CRDB, Catherine Rutenge ambaye ni mkuu wa msafara huo ameahidi kwamba, nasaha za Serikali zitafanyiwa kazi ili kuujenga uchumi wa taifa letu.
“Tutaendelea kutoa fursa ya wateja wetu kujifunza iwe kwa nadharia kuitia semina tunazozitoa maeneo mbalimbali nchini kwetu au kwa safari kama hizi.
Hii ni awamu ya kwanza kwa mwaka huu, baadaye, Oktoba tunatarajia kuja na kundi la pili litakalowajumuisha wamiliki wa shule,” amesema Catherine.
Crédito: Link de origem