top-news-1350×250-leaderboard-1

Majura, Regina wasimulia safari yao na Charles Hilary

Unguja. “Alibarikiwa na kipaji kikubwa cha kutangaza, sauti yake ilikuwa na mvuto kwa kila kipindi, asingeweza kufanya kipindi iwe kwenye michezo au habari za kawaida ukashindwa kufurahia, au ukasikia kipindi kinapwaya,”

Hii ni kauli ya mtangazaji mkongwe wa ndani na nje ya Tanzania, Abdallah Majura anaposimulia namna kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Charles Hilary kilichotokea usiku wa kuamkia leo Mei 11, 2025 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, tawi la Mloganzila jijini Dar es Salaam.

Wakati Majura akisema hivyo, Mtangazaji mwingine, Regina Mziwanda amesema Charles alimtoa kwenye dimbwi la kilio na kusaga meno lakini akamshika mkono akitamani afike mbali.
“Lakini ukweli ni kwamba, amefariki dunia kabla sijafika alipotamani nifike, mbuyu umeanguka ni pigo,” amesema Mziwanda.

Akizungumza na Mwananchi leo Majura amesema licha ya watu wengi kupewa sifa baada ya kufariki dunia, lakini sifa anazopewa Charles anastahili na zinasadifu alichokifanya wakati wa uhai wake katika tasnia ya habari.

Amesema alifanya kazi naye kazi Redio Tanzania mwaka 1988 na alikuwa mtu mwenye ushirikiano mkubwa, hakuwa mchoyo alipenda kile anachokijua kila mmoja akijue.

“Unajua wakati mwingine watu wengi huwa wanawapa watu sifa ambazo sio zao wakishakufa, lakini kwa Charles hiki tunachokisema ni uhakika kabisa alikuwa sio mchoyo, hakuwa mgumu kutoa alichonacho, kutoa elimu na hakuwa mchoyo ukimuuliza chochote, milango yake ilikuwa wazi wakati wote,” amesema Majura.

Amesema alibarikiwa kuwa na kipaji kikubwa cha kutangaza, sauti yake ilikuwa na mvuto kwa kila kipindi asingeweza kufanya kipindi iwe kwenye michezo au habari za kawaida ukashindwa kufurahia, au ukasikia kupwaya,” amesema. 

Amesema licha ya wengi kumjua kwenye kutangaza mpira na akawa mahiri kwenye eneo hilo lakini, amefanya vipindi vingine vingi akitolea mfano wa kipindi kilichokuwa kinaitwa Mpwitompwito Redio Tanzania wakati huo kwa sasa TBC Taifa kwani alikipandisha kwa kiasi kikubwa sana.

Amesema Charles alikuwa akisoma habari mtu hatamani amalize alikuwa ni miongoni mwa watu watatu ambao na yeye Majura walimvutia zaidi katika usomaji wa taarifa ya habari.

Akimuelezea zaidi, amesema alikuwa akitoa ushirikiano mkubwa, akitoa mafunzo, na iwapo akiulizwa jambo lazima atajitoa kuelezea ili mtu aelewe.

Kwa mujibu wa Majura, alipojiunga Radio One mwaka 1995, Charles alikuwa bosi wake na alimuamini sana kwenye kazi hata hivyo licha ya kujua kwamba alikuwa amekamilika kwenye kazi, lakini alikuwa akimkosoa anapokesea na aliendelea kujifunza kwa kiasi kikubwa.

Amesema akiwa Radio One, Charles alianzisha kipindi cha charanga, licha ya muziki huo kutokuwa maarufu kwa Tanzania, lakini kwa kipaji chake na uwezo wake wa kuandaa kipindi hicho, kilitokea kuwa kizuri na maarufu nchini ambacho kilipata mashabiki wengi.

Amesema kupitia kipindi hicho, aliyekuwa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi alipokuwa akisafiri kwenda nje ya nchi alikuwa anarudi na  CD nyingi za muziki huo anampa Charles baada ya kuvutiwa na namna alivyoendesha kipindi kile na kilivyopokewa na wasikilizaji.

Amesema katika usomaji wa taarifa yake, alivutia sana kwa sababu ya matamshi yake na umahiri wake kwenye lugha ya Kiswahili.

“Alikuwa na ulimi, lafudhi Kiswahili kizuri, alikuwa mtaalamu wa Kiswahili, kwa hiyo alipokuwa akichanganya vyote hivyo kilikuwa kinavutia sana,” amesema Mjura.

Kikubwa ambacho kitaendelea kukumbukwa kwake kwa mujibu wa Majura, ni ucheshi. Amesema ilikuwa huwezi kukaa naye kwa dakika tano ukashindwa kucheka, na sio kicheko cha kulazimisha ila ni uhalisia, “kwa hiyo nacho kilikuwa kipaji cha kipeke.”

Amesema kwa Tanzania ni kama imepoteza kidani cha dhahabu katika suala la utangazaji, “Sote ni watangazaji lakini kila mmoja ana kivutio chake kwa wasikilizaji na watazamaji, Charles aliwashika nyoyo wengi.”

Amesema watu wengi walipenda utangazaji wake na alilazimisha kama ni redio mtu amsikilize na kama ni Tv mtu amwangalie, hivyo msiba huo umepokewa kwa masikitiko makubwa na kila mmoja ameshtuka.

Mtangazaji mwingine, Regina Mziwanda amesema anamfahamu Charles kama baba, rafiki na mwongoza njia.

“Charles Hilary alinitoa kwenye dimbwi la simanzi, kilio na kusaga meno wakati nilipopigwa zengwe nikiwa Redio Uhuru bila kujali mizengwe hiyo alisimama kuhakikisha naingia Redio One na kutokea hapo dunia ikanifahamu,” amesema Regina.

Amesema Charles aliwahi kubeba shida za watangazaji wanawake akisema wasiingie zamu za usiku kwa sababu ya kuthamini nyumba na ndoa za watu.

“Ni mtu ambaye alikuwa anaona kwamba huyu akifanya hiki itakuwa taabu basi ni Charles Hilary, ofisini ni bosi mtaani ni rafiki, kwa hiyo unaweza mkakaa popote mkacheka lakini mkiingia studio anakuwa bosi,” ameleza.

Akizidi kusimulia, Regina amesema: “Nakumbuka alinikabidhi kipindi cha ‘Charanga time’ na kipindi cha Kiswahili ambacho kiliniongezea watu wengi kunifuatilia na kunitambua kwenye hilo.”
 

“Licha ya kumueleza kwamba siwezi lakini aliniambia utafanya, kwa hiyo nashukuru kila alichokuwa amenipa nilikifanya akiwa na imani kwamba naweza, yeye ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa sana kuhakikisha nafika hapa nilipofika,” amesema Regina.

Amesema; “ndoto yake aliwahi kuniambia ni kuniona nafika mbali sana lakini kwa isivyo bahati, sijafika alipotamani nifike, ameondoka.”

Mtangazaji huyo wa BBC, amesema tasnia ya habari imetikiswa na Charles ni miongoni mwa watu watangazaji na waandishi nguli walikuwa wamesalia na waliokuwa wakijifunza kutoka kwake sasa hayupo tena.

“Kwa kweli Mbuyu umeanguka, tasnia ya habari tutamkumbuka, mcheshi, mbunifu na mtu mwenye utu wake, na mtu mwenye kauli, mtu anayejua utu, Mwenyezi Mungu amrehemu, ampe kauli thabiti na ampokee, pumzika salama Charles Hilary,” amesema Regina.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.