top-news-1350×250-leaderboard-1

Wabunge CCM wamuangukia Makalla wakidai barabara

Morogoro. Wabunge wa Ulanga na Malinyi wamesema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kupeleka maendeleo katika wilaya hizo,  bado wanakabiliwa na changamoto ya barabara wakimuomba Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla kuisukuma ajenda hiyo ili kuboresha miundombinu hiyo.

Hata hivyo, wameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya kilomita 113 kuanzia Ifakara (Kilombero) hadi Mtimbila wilayani Malinyi zitakazoanza kujengwa mwaka huu.

Endapo kilomita hizo 113 zitajengwa itakuwa kimebaki kipande cha kutoka Mtimbila hadi Malinyi makao makuu ya wilaya cha kilomita 45 na kipande cha kutoka Lupiro njiapanda hadi Mahenge makao makuu ya Ulanga cha kilomita 39.
 

Wabunge hao walieleza hayo, leo Ijumaa Mei 9,2025 wakati wakihutubia kwa pamoja katika uwanja wa Shule ya Msingi Lupiro wilayani Malinyi katika mkutano wa hadhara uliondaliwa maalumu kwa ajili ya Makalla.

Wa kwanza alikuwa mbunge wa Malinyi, Antipas Mgungusi aliyesema Serikali imefanya kazi nzuri ya kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, maji, mawasiliano, umeme na afya, lakini kilio chao kikubwa ni miundombinu ya barabara inayounganisha majimbo hayo.

“Tunaishukuru Serikali kuboresha sekta za afya ikiwemo kuleta magari ya wagonjwa, ujenzi wa hospitali ya Malinyi imekamilika na kuwekewa vifaa vya kisasa, yaani mambo mengi yamefanyika hapa,”

” Shida yetu wananchi wa Bonde la Kilombero ( Ulanga na Malinyi) ni miundombinu barabara. Tunashukuru Serikali imekamilisha kipande cha Kidatu hadi Ifakara, tunaamini mwaka ujao wa fedha tutapata kilomita zingine,” amesema Mgungusi.

Mbunge wa Ulanga, Salim Alaudin ameungana na Mgungusi akisema “Kama ambavyo mbunge mwenzangu amesema tumepata kilomita 113, lakini katika bajeti ijayo zitaongezwa, lakini tunaomba ukalitie msisitizo maana jambo hili limekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Ulanga na linadhoofisha uchumi,” amesema Alaudin.

Katika mkutano huo, Alaudin alitumia nafasi hiyo kukabidhi vifaa vya ujenzi alivyoviahidi katika mikutano yake ikiwemo, mabati na saruji vitakavyopelekwa katika nyumba za ibada, zahanati na shule ili kumalizia ujenzi wa maeneo hayo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Dk Christina Ishengoma alikazia hoja hiyo, akisema,” hili jambo kubwa la Ulanga ni barabara wewe (Makalla) umepita umeona na umerushwa rushwa tunaomba utusaidie kusukuma hii ajenda,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema yaliyosemwa na  wabunge yote yapo sawa na kwamba ndio  ndio kero kubwa ya Ulanga na Malinyi, hata hivyo wamewasiliana na wizara ya Ujenzi kueleza barabara za maeneo hayo zinahitaji nguvu ya ziada.

Katika ziara hiyo, Makalla amesema,” nimekuja kusafirisha njia nitazipeleka changamoto zenu kwa viongozi wakuu, kuanzia kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa).

“Muda wote wakati wabunge wanawasilisha kero hizi, nilishika simu kuwasiliana na Waziri wa Ujenzi (Abdallah Ulega). CCM inawajibu wa kutatua changamoto kwa kuisimamia Serikali, bahati nzuri nimefika huku na nimerushwa rushwa na barabara, nimeona kuona ni kuamini,” amesema.

Kutokana na hilo, Makalla aliwahidi wananchi na wabunge wa Malinyi na Ulanga kwamba atakuwa balozi mzuri wa kupigania changamoto hiyo, tayari Serikali imeshaanza kufanyia kazi kilomita 113.

“Nimezungumza na Ulega wanafanya mapitio ya mwisho ili kutoa fedha za awali kwa ajili ya makandarasi, baada ya ziara yangu atakuja Ulanga na Malinyi asiishie darajani afike hadi Mahenge ajionee barabara ilivyo na arushwe rushwe kama mimi,” amesema.

Makalla amewahakishia wananchi wa Morogoro CCM ina dhamira njema ya kuwatumikia ili kutatua changamoto hizo zinazowakabili ikiwemo tatizo la miundombinu.

Katika mkutano Makalla amemvaa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche akisema wanaondoka katika chama hicho, siyo kwamba wamefika bei au kuhongwa bali wamesoma alama za nyakati kutokana na chama hicho kikuu cha upinzani kukosa mwelekeo.

Jana, akihutubia wananchi wa Karagwe, Heche amewashukia waliokuwa makada wa chama hicho waliotangaza kujivua uanachama akidai wamefika bei.

Katika mkutano huo, Heche aliwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na wanaofika bei na kusaliti imani ya kupigania mabadiliko ya kimfumo kwenye uongozi wa nchi kwa sababu viongozi na makada wa Chadema waliosalia wataendeleza mapambano bila kuchoka wala kurudi nyuma.

Katika maelezo yake, Makalla amesema,”Chadema msitafute mchawi, mchawi nyinyi wenyewe mnaiua Chadema kwa mikono yenu wenyewe, eti anasema hawa wamehongwa…

” Heche usirushe mawe wakati upo kwenye nyumba za vioo, anawatuhuma wenzake wakati yupo kwenye nyumba zao vioo.Leo wanasambaratika na bado, kwa sababu hawatashiriki uchaguzi, hadi kufika 2030 watakuwa choka mbaya,” amesema Makalla.

Hata hivyo, Makalla amewapongeza waliokuwa makada wanaokihama Chadema akiwafananisha na watu wajanja wenye upeo wa kuona mbali.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa amesema kwa sasa chama hicho hakipo tayari kujibishana na mtu wakiwemo makada wao wanaotaka kuondoka na waliondoka wakiwatakiwa kila la kheri.

“Waambie CCM na wengine viongozi wakuu Chadema hatuna muda wa kutafuta mchawi, hatupo tayari kugombana wala kubishana na wanaondoka .Kwa vile wapo tayari kuondoka watumie nafasi hiyo kuondoka, walikuwa wanachama tunaheshimu mchango wao,” amesema.

“Chadema sasa hivi kinajitengeneza upya ili kuaminika kwa umma katika kupigania mambo ambayo wananchi wanayahitaji, hatupo katika kutafuta mchawi,” amesema Golugwa.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.