Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kuwakamata na baadaye kuwaachia kwa dhamana viongozi na wafuasi watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaodaiwa kujihusisha na mkusanyiko katika eneo la Mahakama ya Kisutu wakati wa kusikilizwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Tukio hilo limetokea mapema leo Alhamisi, Aprili 24, 2025, ambapo kulikuwa na idadi kubwa ya vikosi vya usalama katika eneo hilo kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni hatua za kiusalama ikidaiwa kuwa kuna taarifa za uwezekano wa vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa: “Kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu inaendelea kwani hilo ndilo jukumu kubwa la msingi la Jeshi la Polisi.”
Polisi imewataja watu waliokamatwa kuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, Katibu Mkuu, John Mnyika, Chacha Heche Seguta, Swezi Dani Naradufu na James Mseti.
“Baada ya mahojiano, dhamana zao ziko wazi. Jeshi linatoa wito kwa wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya kihalifu kwani halitakuwa na huruma, lakini litashughulikia kwa kufuata misingi ya kisheria,” imeeleza taarifa hiyo ya polisi.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na kazi ya kuhakikisha usalama wa Jiji unadumishwa na litachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayejaribu kuvuruga amani, hasa katika maeneo yenye mvutano wa kisiasa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa uwepo wa viongozi hao katika eneo la Kisutu ulikuwa ukifuatilia mwenendo wa kesi ya Tundu Lissu, lakini hatua zao zilitafsiriwa kama kikwazo kwa taratibu za usalama zilizokuwa zikiendelea katika eneo hilo.
Crédito: Link de origem