Dar es Salaam. Sakata la mabinti wa chuo wanaotuhumiwa kumdhalilisha mwenzao limechukua sura mpya baada ya Serikali kuagiza mtu aliyetajwa kwa jina la Mwijaku ahojiwe na Polisi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima ambaye amesema, mtu aliyetajwa kwa jina la Mwijaku kwenye kipande cha video inayosambaa kwenye mitandao, atahojiwa na Jeshi la Polisi.
Katika video hiyo iliyoanza kusambaa usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka, Aprili 20, 2025 inaonekana msichana ambaye jina lake bado halijatambulika akidhalilishwa, kupigwa na wahusika wanaodaiwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku wakimtaja mhusika kwa jina moja la Mwijaku.
Video hizo ziliibua mijadala mitandaoni jambo lililomfanya Waziri Gwajima kuingilia kati na kuagiza hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Tayari UDSM na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wamekwisha kutoa taarifa za kulaani tukio hilo.
Leo Jumatano, Aprili 23, 2025, Waziri Gwajima ametoa taarifa kwa umma kuhusu sakata hilo huku akisema Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hao naye atahojiwa kwa mujibu wa sheria.
“Jeshi letu la Polisi linaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria kuhusu kuwahoji wahusika wa tukio hilo. Kwa upande mwingine, jamii nayo imeendelea kuhoji mbona aliyetajwa kuwa ni Mwijaku hakamatwi?
”Ndugu wananchi, napenda kuwahakikishia kuwa Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hao, naye atahojiwa kwa mujibu wa sheria. Baada ya hapo wizara yangu itaona nini ifanye kuhusu mustakabali mzima wa maadili ya jamii na nafasi ya huyo Mwijaku na wengine wote wenye nafasi zenye kuchochea kasi ya athari chanya au hasi kwenye maadili ya jamii,” amesema Waziri Gwajima.
Amesisitiza wananchi kuwa watulivu huku wakiendelea kufuatilia taarifa za Jeshi la Polisi.
Jumatatu ya Aprili 21, 2025 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro akizungumza na Mwananchi alisema wanafuatilia tukio hilo. Jitihada za kumpata leo kujua kinachoendelea hazijazaa matunda.
Crédito: Link de origem