Dar/Mikoani. Ikiwa imesalia takribani miezi sita Tanzania kuingia katika uchaguzi mkuu, viongozi wa dini wametoa wito kwa Serikali na wadau wa siasa kuhakikisha unakuwa huru na wa haki, wakisisitiza kuwapo mabadiliko ya mifumo kabla ya uchaguzi, huku wanaoshikiliwa waachiwe huru pasipo masharti.
Kwa nyakati tofauti wakihubiri wakati wa mkesha wa Pasaka, Aprili 19 na sikukuu yenyewe Aprili 20, 2025, wamesisitiza uchaguzi mkuu ujao haupaswi kuwa chanzo cha migogoro, bali njia ya kupatikana viongozi wa haki, wa kweli na wazalendo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mamlaka yoyote halali lazima itokane na ridhaa ya watu, kwa msingi huo wamehimiza wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu kwa kuwania nafasi zilizopo na pia kupiga kura.
Kuhusu waumini wanaowania uongozi, wamefungua milango kwa wanaotaka kushiriki mchakato huo wa kisiasa kwenda kuombewa.
Mbali ya hayo, wameiasa jamii kuendelea kuishi maisha ya uaminifu, sala, huruma na mshikamano kama walivyoishi katika kipindi cha Kwaresma, wakitakiwa kuwa na msimamo wa maadili, kuachana na matendo ya giza kama ufisadi, dhuluma, ubaguzi na chuki.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang Pisa, amesema ni muhimu Serikali kukaa na wadau wa uchaguzi, kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Askofu Pisa, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesisitiza umuhimu wa amani kuelekea uchaguzi huo, akitaka wote waliokamatwa kwa kudai mageuzi ya mifumo ya uchaguzi waachiwe haraka na bila masharti.
Askofu Pisa ametoa wito huo wakati ambao wadau wa haki wanashinikiza kuachiwa huru Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), Tundu Lissu aliyekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 alipokuwa ziarani kuhamasisha ajenda ya No reforms, no election wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Alihamishiwa kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam, baadaye akafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Askofu Pisa katika mahubiri ya misa ya mkesha wa pasaka kwenye Kanisa la Mtakatifu Andrea Kaggwa, mkoani Lindi, moja kati ya mapendekezo yake manne kuelekea uchaguzi, amesema wahusika wakae na wadau wote kuruhusu mabadiliko ya lazima kabla ya uchaguzi mkuu.
Amesema sauti na vilio vya wengi vinapaswa kusikika akisisitiza: “Kasoro zilizojitokeza zinapaswa kurekebishwa haraka. Kukiwa na nia ya dhati kutoka kwa wahusika muda unatosha kabisa kufanya hayo marekebisho kabla ya uchanguzi mkuu.”
Akizungumzia amani, amehoji nani anayeiharibu kati ya anayetumia nguvu kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka na yule anayeshauri kukaa mezani kufanya mabadiliko ya mifumo.
“Katika hali ya kawaida nani anaharibu amani, anayetumia nguvu na kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka yeye au yule anayesema jamani turudi mezani ili tuangalie mifumo yetu ya uchaguzi, kwani kwa mfumo wa sasa hauwezi kutupatia viongozi wa haki na wa kweli?” amehoji.
Ametaka wote waliokamatwa kwa kudai haki wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani waachiwe haraka na bila ya masharti.
Askofu Pisa amesema kusitokee wengine watakaokamatwa au kusumbuliwa kwa namna hiyo.
“Tuiombee nchi yetu, iwe nchi ya amani na kuwa na viongozi wa haki na wazalendo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Askofu Pisa amesema kwa misingi ya demokrasia, mamlaka ya Serikali yanatokana na iliyochaguliwa kihalali, akieleza katika demokrasia ya kweli viongozi watawajibika kwa wapigakura.
“Kura ni wakala wenye nguvu, wananchi wasiporwe nguvu yao ya kupiga kura na kuchagua,” amesema.
Amesema hoja zinazoibuliwa na wadau hazionyeshi kupatikana kwa uchaguzi wa haki na kweli, hivyo ni muhimu zizingatiwe ili kupata suluhisho.
Askofu Pisa amesema kukiwa na uchaguzi wa haki, viongozi watakaochanguliwa watakuwa tunda la haki na ukweli.
Kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, amesema unatokana na malalamiko ya uchaguzi wa mwaka 2019, 2020 na 2024, yanayodai haukuwa wa halali wala wa haki.
“Unamhakikishiaje mwananchi huyo kwamba uchaguzi mkuu utakuwa wa halali? Tangu uchaguzi wa Serikali za mitaa ufanyike, bado hata miezi sita haijapita,” amesema.
Amesema kwa bahati mbaya bado kasoro zilizobainishwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba, 2024 hazijarekebishwa wala kujibiwa.
Amesema tayari mapendekezo kuhusu muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yalishatolewa, hivyo ni muhimu yatekelezwe.
Ametaka mihimili isiingiliwe, iachwe itende kazi zake kwa haki. Amesema watu wasipochagua kwa uhuru, demokrasia itakufa.
“Madikteta wengi duniani na hata hapa Afrika hawataruhusu uchaguzi ufanyike kwani wanaogopa uchaguzi ukifanyika hawatachaguliwa. Kama wataruhusu uchaguzi wataharibu mifumo ili wabaki madarakani. Tanzania hatujafika huku,” amesema.
Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesisitiza maridhiano, uchaguzi huru na haki na uamuzi wa wananchi katika uchaguzi kuheshimiwa.

Askofu Shoo amesema wakati akitoa ujumbe wa Pasaka katika kanisa kuu, Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia maridhiano, Dk Shoo amesema yanapaswa kuingia katika matendo na si kubaki kuwa maneno.
“Tunasikia habari za mapigano, migogoro kila mahali kati ya makundi, kati ya nchi na kati ya mtu na mtu, tunasikia habari za ukatili na uonevu kwa wasio na nguvu na mamlaka, mahali pengine inaelekea kushamiri tena hata hapa kwetu,” amesema.
Amesema kunahitajika kupatana, kuridhiana na kupendana.
“Tunaposema juu ya upatanisho tunamaanisha, tunaposema juu ya kuridhiana tunamaanisha, tunaposema juu ya kujenga upya, kuleta mabadiliko yatakayofanya watu wote waweze kuishi kwa amani na haki itendeke na kuletea nchi yetu maendeleo tunamaanisha. Tunapozungumza kuhusu ustahimilivu siyo maneno maneno tu, bali sisi kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu Kristo tunakuwa vyombo na wajumbe wa mambo haya,” amesema.
Hata hivyo, Dk Shoo akizungumzia uchaguzi mkuu amesema ni haki na wajibu wa raia kujichagulia viongozi wanaowataka, akionya wananchi wasiingiliwe wala kuzuiwa kuwachagua viongozi wawapendao.
“Tunaomba uchaguzi huu usifanane na chaguzi zilizopita, ule wa 2019, 2020 na huu uluofanyika mwaka jana. Tumerudia mara nyingi na mahali pengi, hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi hizi nilizotaja yakijirudia.”
Dk Shoo pia amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha hawatumiki vibaya katika uchaguzi kwa masilahi ya watu wachache.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani wakati akiongoza ibada ya Misa takatifu ya Pasaka iliyofanyika katika kanisa kuu la roho Mtakatifu Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Katika hilo, Askofu wa Kanisa la Aglikana Tanzania Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuongeza jitihada za kuondoa kero zilizopo kwa wananchi zinazochangia Watanzania kutajwa kama watu wasio na furaha, akieleza ni wakati sasa kwa Serikali kukaa meza moja na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kumaliza tofauti zilizopo kwani hazina afya kwa maendeleo ya Taifa.
Askofu Chilongani akihubiri katika ibada ya Pasaka kwenye Kanisa Kuu la Anglikana la Roho Mtakatifu amehoji ni kwa nini pande hizo ziendelee kulumbana ilihali wanaweza kukaa meza moja wakayajenga.
“Siwezi kusema nani yuko sawa na nani hayuko sawa lakini kwa masilahi ya Taifa letu niombe Serikali yangu kukaa meza moja na Chadema ili wayamalize kwani bila kufanya hivyo tutatumbukia katika maeneo ambayo si salama,” amesema.
Amesema kuna mambo mengi yanayosababisha kukosekana furaha, baadhi yakiwa ni ubadhirifu, rushwa na ukiritimba katika ofisi za umma.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malalusa akizungumza katika Usharika wa Azania Front wakati wa ibada ya Pasaka, amesema kanisa linafurahi washarika wake wakishiriki kwenye mambo ya kijamii, ukiwamo uchaguzi.

Askofu Malasusa amesema kama wanajamii, Wakristo wana haki ya kupiga kura au kupigiwa kura utakapofika wakati wa uchaguzi, hivyo kushiriki kwao kwenye mchakato huo isiwe kwa kujificha.
“Wanaotaka kutia nia njooni kanisani tutawaombea, Mungu awaongoze katika safari hiyo. Kama una wito basi njoo uombewe ili Mungu akuwezeshe kutafakari,” amesema.
Pia, amewasisitiza Wakristo kote nchini kuwajibika katika kutunza amani ili utulivu na mshikamano uendelee kutawala.
Mtume Boniface Mwamposa wa Kanisa la Inuka Uangaze ametoa wito kwa Watanzania kuliombea Taifa liwe na amani kuelekea uchaguzi mkuu.
Amesema Pasaka maana yake ni wokovu, uponyaji, ushindi, maangamizo na amani, hivyo katika Taifa la Tanzania kitu pekee cha kulilinda ni amani.
Kwa mujibu wa Mwamposa, kipindi cha uchaguzi kinakuwa na mambo mengi na adui ndipo anapofungulia malango ya aina mbalimbali ya makabila na dini, hivyo ametaka wawe sehemu ya amani katika Taifa.
Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Nyanda za Juu Kusini, Dk Edward Mwaikali amesema muda wa kuliombea Taifa kuendelea kuwa salama ni sasa kutokana na tukio kubwa la uchaguzi mkuu.
Amewaomba Wakristo, wakiwamo waumini wa Usharika wa Ruanda, jijini Mbeya kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kugombea urais, ubunge na udiwani.
Akisisitiza kuhusu amani amesema: “Hii amani iliyopo viongozi wa Serikali wamejitahidi sana, lakini isitoshe watumishi wa Mungu wa dini zote wamehusika. Tushikilie amani yetu tuvuke kwa pamoja, tusijifananishe na baadhi ya mataifa ambayo vita na migogoro imetawala.”
Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu katika mkesha wa Pasaka, amewasihi waumini kutenda matendo ya mwanga na ya haki, badala ya ufisadi, dhuluma na unyanyasaji.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki teule la Bagamoyo, Stephano Musomba amesisitiza waumini kutoacha aina ya maisha waliyoishi katika kipindi chote cha mfungo wa Kwaresma.
Akihubiri wakati wa mkesha wa Pasaka amesema: “Kama tulivyosafiri na sala, kufunga, kutoa sadaka na matendo ya huruma katika kipindi cha Kwaresma, vivyo hivyo tuendelee hata sasa.”
Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel Kibaha, mkoani Pwani, Exavia Mpambichile pia amesisitiza amani kuanzia ngazi ya familia, huku Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Isaya Chambala akisema amani ya kweli haiji bila haki, hivyo kuwataka viongozi wanapohubiri amani kukumbuka kutenda haki.
Akihubiri wakati wa ibada ya sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Anglikana Mkunazini, Unguja amesema:”Amani ya kweli haiji bila haki, pale penye dhuluma, unyanyasaji, ubinafsi haiwezi kuwapo amani. Lazima tuhakikishe unapotafuta amani yako, tafuta amani ya wengine bila kuleta ubaguzi na kufanya dhuluma.”
Amevitaka vyama ambavyo vimepewa jukumu kikatiba la kuteua wagombea, kuleta watu ambao ni waadilifu na wananchi watumie nafasi yao kusema ndiyo au hapana kwenye boksi la kura.
Askofu wa Kanisa la Zanzibar International Christian Center (ZICC), Donath Kaganga amewataka wananchi na viongozi kuendesha uchaguzi wa haki na amani, akiwaasa vijana ambao mara nyingi wanatumika kueleza mambo yanayoweza kusababisha fujo.
“Tunawaasa vijana waende katika mikutano kwa lengo la kusikiliza sera na siyo kufanya fujo, unapotumika kuharibu amani watakaoathirika siyo chama fulani wala dini fulani ni watu wote,” amesema.
Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel amevitaka vyama vya siasa na Serikali kila mmoja kwa nafasi yake kutenda haki kwani haki huinua Taifa.
Crédito: Link de origem