Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Anthony Komu, amerejea kwenye chama hicho baada ya kuhamia NCCR-Mageuzi.
Itakumbukwa kuwa Komu alikuwa miongoni mwa makada wa Chadema walioingia kwenye mzozo, na kusababisha ahojiwe kabla ya kujiondoa.
Komu ametambulishwa leo, Aprili 19, 2025, na Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche, wakati wa mkutano wa hadhara wa kusambaza elimu ya kampeni ya Chadema ya No reforms, no election (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi), uliofanyika Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Kwa nyakati tofauti, akiwa Chadema, Komu mbali na kuwa mbunge wa Moshi Vijijini (2015–2020), pia amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Fedha. Akiwa NCCR-Mageuzi, Komu amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.
Awali, akihutubia katika mkutano huo, Heche, amesema tatizo linaloisumbua Tanzania ni ukosefu wa siasa safi na uongozi bora.
Amesema chama hicho kimejitolea kupigania hilo ili Watanzania wanufaike kupitia rasilimali zilizopo na waishi maisha bora.
“Mabadiliko makubwa duniani huletwa na vijana wanaoishi mijini. Ni wakati wa vijana kuwa mstari wa mbele kutuunga mkono kupitia kampeni yetu ya No reform, no election. Tubadilishe mambo, tupate viongozi bora na tuweke mfumo wa siasa safi.
“Tunatakiwa kuikataa hii hali ya unyonge. Ni muhimu wananchi wakaamua kuisimamia Serikali kwa kupata viongozi wanaojua shida za wananchi,” amesema Heche.
Amesema chama hicho kupitia kampeni yake hiyo, kinaamini muafaka utapatikana, huku akisisitiza mabadiliko.
“Kiungeni mkono chama hiki, kina dhamira ya kweli katika kubadilisha maisha ya Watanzania. Chadema ni ishara ya utajiri, kina sera zinazokuja kutibu shida mnazopitia,” amesema makamu huyo mwenyekiti.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Rose Mayemba, amesema viongozi wa chama hicho wamejitolea kuzunguka mikoa yote kuwaambia Watanzania kuwa bila mabadiliko, hakuna uchaguzi, na wapinzani wao walidhani hawawezi kufanya hivyo.
“Tulianza kama mzaha, sasa dawa imeanza kuwaingia, na matokeo yake, wameanza kutuwekea vikwazo viongozi wetu ili kudhoofisha safari yetu ya kudai mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi,” amesema Mayemba.
Kada ambaye pia aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Charles Odero, amesema Watanzania wengi wanapitia ugumu wa maisha, ndiyo maana wakienda kwenye migahawa kabla ya kuagiza chakula, wanaulizia bei.
“Hizo ni dalili za umaskini. Watanzania hawana furaha ya maisha na wengi wao hawana wanachomiliki na yote hayo yanasababishwa na ukosefu wa uongozi wenye dira. Na tambueni, Katiba yetu ya mwaka 1977 inasema mamlaka yote ya nchi yanatoka kwa wananchi,” amesema Odero.
Odero amesema Serikali inawajibika kuangalia ustawi wa wananchi wake na kuwainua kiuchumi, kiafya, kijamii, na kuwapa haki msingi wanazostahili ili waondokane na adha nyingine zinazowakumba kimaisha.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tegeta Kibaoni, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, amekazia suala la chama hicho kutoshiriki uchaguzi hadi mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi yatakapotekelezwa na Serikali.
Jacob, maarufu ‘Boni Yai’, amesema No reforms, no election ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi.
“Tunataka kuingia kwenye uchaguzi ambao watu hawakimbii na masanduku ya kura au mawakala wa upinzani, wakiwemo Chadema, wanatolewa nje ya vituo vya kupigia kura,” amesema Jacob.
Crédito: Link de origem