top-news-1350×250-leaderboard-1

Shahada masomo ya kichina sasa kufundishwa UDSM

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinatarajia kuanzisha shahada nyingine itakayojikita katika masomo ya Kichina na Kiswahili lengo likiwa kuongeza wigo na fursa ya soko la ajira.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 18, 2025 na Naibu Makamu  Mkuu wa Chuo Taaluma hicho, Bonaventure Rutinwa, katika ufunguzi wa mashindano ya awali ya lugha ya  Kichina kwa mwaka 2025 yanayofanyika chuoni hapo na kuratibiwa na Taasisi ya Confucius ya chuoni hapo.

Rutinwa amesema hatua hii inakuja ikiwa tayari chuo hicho kumeshaanzishwa shahada ya awali ya  ya elimu katika  lugha ya kichina na kingereza.

Amesema shahada hiyo itafundishwa kwa wanafunzi wanaosoma shahada ya awali ya ualimu katika kichina na Kiswahili chuoni hapo na itatolewa na taasisi hiyo ya Confucius kwa kushirikiana na chuo cha UDSM.

Akisoma risala kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shahada za uzamili UDSM, Profesa Rose Upor, amesema Taasisi ya Confucius imekuwa kiungo muhimu katika ufundishaji wa lugha na utamaduni na kukuza ushirikiano baina ya China na Afrika.

“Wakurugenzi wa Confucius kutoka bara la Afrika wamekuwa wakifanya jitihada  kuhakikisha vijana wengi wanajifunza lugha ya Kichina ambacho kinawapa fursa ya kushiriki katika soko la ushindani.

Mkurugenzi wa Shahada za uzamili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rose Upor

 Akifafanua zaidi kuhusu hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius Dk Musa Hans amesema wameamua kuja na shahada hiyo baada ya kuwepo kwa uhitaji.

“Hivi sasa kumekuwa na kampuni nyingi za Kichina zinazofanya kazi hapa nchini hivyo kumekuwa na uhitaji wa wafanyakazi Watanzania wanaotakiwa kufanya kazi huko, kipaumbele kikiwa kujua lugha hiyo ya kichina,”amesema Dk Hans.

Ni kutokana na uhitaji huo, amesema wamekuwa wakiwahimiza hata wanaosoma kozi nyingine zikiwemo za uhandisi na ujenzi kujifunza lugha hiyo kwa kuwa itawasidia kupata ajira kirahisi kwenye kampuni za ujenzi ambazo zimekuwa zikishinda zabuni katika miradi mbalimbali hapa nchini.

Aidha Mkurugenzi huyo amewahimiza pia wanaomaliza kidato cha nne au cha tano kwa muda wanaokuwepo nyumbani wakisubiri matokeo kujitahidi kujifunza lugha hiyo ili hata watakapoingia vyuoni na kukutana nayo inakuwa rahisi kuendelea kujifunza.

“Kwa sasa hapa mbali ya kufundisha shahada pia tunafundisha kozi fupifupi kwa kuwa wanaosoma shahada ya kichina ni wale waliosoma lugha hiyo pia wakiwa kidato cha tano na sita.

“Lakini kama mtu ataanza kuisoma kidogokidogo mbele ya safari anaweza akajiendeleza kuisoma zaidi,”amesema Dk Hans.

Akizungumzia kuhusu mashindano hayo, Profesa Upor amesema yanasaidia kuwatia hamasa  wanafunzi wengine wapende kujifunza lugha hiyo  na wale ambao tayari wanasoma itawaongezea bidii katika ujifunzaji wao.

Wakati Profesa akiyasema hayo, Dk Hans amesema tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2002, mpaka sasa zaidi ya wanafunzi milioni 1.5 kutoka zaidi ya nchi 150 wameshiriki na kuonyesha mafanikio ya katika kujifunza lugha hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Mwambata wa masuala ya utamaduni kutoka ubalozi wa China nchini Tanzania, Xu Yongliang, amesema zaidi ya nchi 180 zinafundisha kichina na karibu watu milioni 200 nje ya China wanajifunza lugha.

 “Tunatarajia wanafunzi waendelee kujifunz  kwa bidii, walimu wazidi kung’ara na jamii  kuinga mkono Taasisi ya Confucius,”amesema  Yongliang.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius, Profesa Zhang Xiaozhen amesema mashindano hayo yamewahusisha wanafunzi kutoka Taasisi ya Confucius Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na Chuo cha Uhusiano wa Kidiplomasia.

Profesa Zhang amesema wanachoangalia ni upimaji katika uimbaji, ughani wa mashairi,kung fu, uelewa kuhusu nchi ya China pamoja na maonyesho ya vipajji mbalimbali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi walioshiriki mashindano hayo, akiwemo Aisha Yahaya, kutoka UDSM amesema amejisikia faraja kushiriki mashindano hayo ambayo yamemsaidia kujijenga katika kujiamini kusimama na kujieleza mbele za watu.

Neema Joanes, amesema anavutiwa kusoma kichina kwani amekisoma kwa miaka nane tangu akiwa kidato cha kwanza huku akiwataka wengine kujifunza kwa kuwa kina fursa nyingi ikiwemo ajira.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.