Dar es Salaam/mikoani. Kilio cha haki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2025, ni miongoni mwa mambo yaliyochukua nafasi kubwa kutoka kwa viongozi wa dini ya Kikristo nchini, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wao katika mahubiri ya Ibada ya Ijumaa Kuu.
Wameambatanisha ujumbe huo na msisitizo kwa Watanzania kuhakikisha wakati huu wa kuelekea uchaguzi, wanatumia fursa za kidemokrasia kufufua matumaini ya kujenga nchi ya haki na kutetea wanyonge.
Sambamba na hayo, wamewataka wasaidizi wa viongozi kuacha kuwapotosha, huku wakidokeza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuacha tabia ya kukosoa kila kitu hata mazuri yanayofanywa na Serikali, kadhalika Serikali nayo ikubali kukosolewa ili ijirekebishe kwa maslahi ya wananchi wake.
Hoja zimeibuliwa na viongozi hao wa kiroho, ni sehemu ya zile ambazo aghalabu zimekuwa zikisikika kutoka katika vinywa vya wanasiasa wakishinikiza haki na usawa kwenye mifumo ya uchaguzi nchini Tanzania.

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo
Katika kushinikiza hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaendelea na kampeni yake ya No Reforms, No Election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi), wakishinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi na sheria ili vyama vya siasa viwe na uwanja sawa.
Kwa upande wa vyama vingine vya siasa, kikiwamo ACT Wazalendo, CUF, licha ya kuweka wazi dhamira yao ya kushiriki uchaguzi, msisitizo wao ni kuwepo haki ndani ya mchakato huo.
Kunyamazisha watu hakunyamazishi malalamiko
Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo katika Ibada ya Ijumaa Kuu kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Ifakara mjini, Dayosisi ya Ulanga Kilombero, amesema kukamata watu na kuwaweka ndani hakunyamazishi malalamiko yao, bali kunaendelea kuongeza mwanya wa kuonekana zaidi.
Badala ya kutumika kwa njia hiyo, Askofu Mameo amesema ni muhimu kumpuuza mtu na kuendelea kusimamia misingi, akitolea mfano maandamano ya Chadema yaliyofanyika nchini na Jeshi la Polisi kuyalinda na yakafanyika kwa amani.
“Wakati mwingine tunaichanganya Serikali ifanye yale isiyotaka kufanya ili tulete vurugu, katika Taifa hili hatutaki vurugu, tumepata uhuru bila kumwaga damu, mgawanyiko katika taifa huleta maadui wa nje,” amesema.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira tayari amewahakikishia Watanzania kwamba chama hicho hakina chuki wala kisasi na mtu, bali kinaamini katika kutekeleza sera ya maridhiano. Alisema CCM inaamini katika maridhiano ambayo pia ni sera ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Niwasaidie tu kuwaelimisha kwamba, mkiwa na sera ya maridhiano haiwi mbadala wa sheria na wala huwezi kusema kwa sababu wewe ni mwenyekiti basi upo juu ya sheria,” amesema Wasira.
Bagonza na haki mwaka wa uchaguzi
Katika salamu zake za Ijumaa Kuu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amewataka Watanzania kuhakikisha mwaka wa uchaguzi, wanatumia fursa za kidemokrasia kufufua matumaini ya kujenga nchi ya haki na kutetea wanyonge.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza
Amewasisitiza kutumia fursa hiyo, ili kuepuka Serikali isigeuzwe kuwa gulio la kuuza na kununua haki za wanyonge.
“Tunaalikwa kuwa chachu ya haki iletayo amani katika taifa letu. Haki inatosha kuleta na kutunza amani. Tuukatae uzushi wa kuimba wimbo wa amani isiyotokana na haki,” amesema.
Kwa mujibu wa Askofu Bagonza kupitia salamu zake hizo, kifo cha Yesu kilibadilisha dhuluma kuwa haki, giza kuwa nuru, kilirejesha matumaini kutoka hali ya kukata tamaa.
“Yote matatu tunayo katika jamii yetu, dhuluma, giza na kukata tamaa. Kumbe basi, Yesu anatualika sote tuupokee ufufuko ili dhuluma iondoke na haki itawale, giza la mioyo lifukuzwe na nuru ya Kristo iangaze na waliokata tamaa wajazwe nguvu mpya,” amesema.
Katika andiko lake hilo, Askofu Bagonza alikwenda mbali zaidi na kueleza, haijalishi utakufa kwa kutekwa, kuliwa na simba au mamba, bali Kristo amekupa uhakika wa uhai na kukutana uso kwa uso na watesi na wauaji wako.
Ujumbe wa haki, pia ulitolewa na Askofu Mameo akisema ingawa dhamira ya siasa za vyama vingi ni kulinganisha sauti, kinachofanyika sasa ni kinyume chake, atakayezidiwa sera atatumia nguvu kumzima mshindani wake.
“Vyama vingi ni sawa na kwaya zinazoimba, kila mtu aimbe wimbo wake mzuri na mtu achague aende anakotaka, hatulazimishi watu kwenda wasipotaka. Wimbo mzuri ndio unaovutia watu na waje kwako, hatulazimishi kwa fimbo na bakora waimbe wimbo unaotaka wewe,” amesema.
Askofu Mameo amesema demokrasia ni kuwapa watu uhuru wa kuwachagua wale wanaowataka, akisisitiza vyama kuwa na sera na malengo ya nini wanataka kuwafanyia wananchi.
Askofu huyo alitoa mfano, akimrejelea Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba aliuliza kwa nini watu wanakimbilia Ikulu, Ikulu ni mahali patakatifu.
“Sasa mnataka kugeuza Ikulu kuwa mahali pa lawama, ni kulaumu tu hata kazi nzuri zinapofanyika,” amehoji.
Askofu Mameo amesema manung’uniko kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi ni kilio katika taifa na malalamiko ya chaguzi zilizopita kutokuwa huru.
Amesema uchaguzi huru ni ule ambao kila mtu anaridhika kushindwa kwa halali, akiomba watawala waliangalie hilo, kwa kuwa malalamiko hayo yanaligawa taifa.
“Haya yanayolalamikiwa siyo ya kutuleta pamoja, ni kutugawa pia, ukigawa taifa nguvu inagawanyika, tunaotaka tume huru tuwe wastaarabu katika kukosoa, tusikosoe hata yale mazuri yanayofanyika, bali kosoeni yale mnayoona hayako sawa,” amesema.
Askofu huyo ametoa wito kwa vyama vya siasa kutoliingiza taifa kwenye migogoro, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia falsafa ya Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4R) ya Rais Samia.
“Msituingize katika migogoro isiyo na sababu, kuna 4R alizoleta Rais Samia, haya yanatuleta pamoja kujadili mambo yetu na kukubaliana hakuna Serikali iliyokamilisha kila kitu,” amesema.
Amesema yapo mapungufu yaliyofanyiwa kazi, huku akidokeza umuhimu wa yale yaliyotekelezwa, japo madogo lakini viongozi wawe na moyo wa kushukuru.
Amesema ni kawaida ya Waafrika kutojua kukosolewa, na ikifanyika hivyo wanachukia, akidokeza: “Kila tunapokosolewa tunaonyeshwa madhaifu yetu na madhaifu yetu ndiyo tunapaswa kushughulika nayo ili yule anayesema akose la kusema.
“Lakini tukiwatishia, kuwakamata tunaleta mwanya na mgawanyiko katika taifa letu zuri ambalo limekuwa mstari wa mbele kuyakomboa mataifa mengine. Ni muhimu kurudia misingi yetu, tusiwe wanafunzi wa siasa,” amesema.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Kardinali Protase Rugambwa amewataka Watanzania kushiriki siasa safi kwa kuepuka kelele, kutukanana na kubaguana kwa namna yoyote, ile ili jamii iishi mazingira bora ya furaha.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Kardinali Protase Rugambwa.
Amesema huu ni wakati ambao Wakristo na Watanzania kwa jumla wanapaswa kushikamana katika kudumisha amani ya nchi kwa kutanguliza upendo kama Yesu Kristo alivyokuwa na upendo.
“Tunayafanya haya yote lakini tunapaswa kufanya zaidi hasa kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, wananchi wanapaswa kuliombea Taifa na ili tuweze kuvuka salama,” amesema Askofu Rugambwa.
Hata hivyo, amesema siyo dhambi kwa watu wenye nafasi ya kushiriki siasa, isipokuwa matendo na mienendo yao iendane na huruma na jinsi watakavyolijenga Taifa kwenye mshikamano.
Amesema katika mafundisho ya imani ni wajibu wa wananchi wote kwenda kuendeleza yale mema na kuondoa mabaya, hasa katika siasa na uchumi ili kudumu katika upendo usiobagua kama ambavyo Yesu Kristo hakubagua hata wale wabaya.
“Kanisa linatoa wito kwa watendaji wa Serikali kutomdanganya Rais, watendaji wa Serikali aisee wanakosea sana, kila Rais anapofika mahali wanamwambia hatukudai, umeleta Sh700 bilioni za maji, Sh500 bilioni za barabara, lakini katika miji yetu baadhi ya barabara hazipitiki na hapo Rais hawezi kupita kila mahali,” amesema Askofu Mameo.
Amesema ni vyema kueleza mengi yaliyofanywa, bila kuacha kusema mapungufu, kwani kufanya hivyo ndiyo ukweli na siyo kumdanganya akaamua ashughulikie mengine akiamini yanayotajwa amemaliza.
Matibabu kwa wazee/rushwa
Kiongozi huyo amesema licha ya kuwepo kwa sera ya matibabu bure kwa wazee, kumekuwa na kilio kwa kundi hilo kupata matibabu, licha ya kulitumikia taifa hili kitambo.
Mbali na hilo, amegusia suala la rushwa, akisema Tanzania imekuwa kama haina kitengo cha kuzuia dhambi hiyo, hasa wakati wa uchaguzi.
Amesema watu wanakula rushwa na kulala nazo, akidokeza kama wanafanya hivyo zipo toba wanazopaswa kutubu.
“Hata kanisani nako rushwa inatajwa, hata mahali patakatifu mnadiriki kuleta rushwa Mungu hapendi, wala rushwa hawatendi haki, hata tunaosema ni watekaji, wasiojulikana sisi tu ndio hatuwajui, Mungu anawajua na watatoa hesabu kwa kuteka watu na kuumiza watu.
“Tunaomba taifa letu lirudi kwenye misingi ya haki liangalie hawa watu wanaosemekana wanapotea na hawapatikani,” amesema.
Akizungumzia suala la rushwa wakati wa uchaguzi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania-CCT, Dk Moses Matonya aliwataka wananchi wasipokee rushwa, kwani kufanya hivyo ni kuuza haki yao ya kupata viongozi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania-CCT, Dk Moses Matonya
“Watu wameanza kukosa uadilifu, wanapokea sana rushwa, jambo ambalo litamkosesha mhusika maendeleo kutokana na kuuza haki yake kwa mtu asiyefaa,” amesema.
Pia amehimiza vyama vyote vina haki ya kupigiwa kura na si sahihi kwa mgombea yeyote kushawishi watu wasikichague chama fulani, kwani kila mtu ana haki ya kumchagua mtu anayeona anafaa bila kuangalia chama.
Dk Matonya amehimiza Watanzania kujiandikisha na kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi bora.
“Tupate viongozi wazuri wenye uzalendo wa nchi yetu na wenye moyo wa kuwatumia Watanzania kwa upendo,” amesema.
Pia, amesema wakati wa uchaguzi ndio shetani hujiinua, hivyo ni muhimu kuombea uchaguzi mkuu na kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura kuhakiki taarifa zake na kujiandikisha katika daftari la wapigakura.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga amesema kwa sasa tunu ya mtu kujitolea kwa ajili ya wengine imepotea, akiomba watumishi wakiwamo wa umma kurejesha utamaduni huo.
Katika mahubiri yake, amesema baadhi ya watu hawataki kuteseka kwa ajili ya wengine.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga
Amesema kama Yesu aliteswa kwa ajili ya dhambi za wanadamu, watumishi wakiwamo wa umma nao kama watajituma kwa ajili ya wengine, watarejesha upya tunu hiyo kwa maslahi ya Taifa.
“Tushike sana maungamo yetu, baadhi hawataki kuteseka kwa ajili ya wengine, utasikia wanasema kila mmoja abebe msalaba wake, hii si sawa, kwani Yesu aliteseka kwa ajili ya dhambi za wanadamu,” amesema Askofu Nyaisonga.
Askofu huyo amesema kupitia mateso ya Yesu Kristo msalabani, waamini wa Kikristo wanaimarika kiimani; “Na wanajikinga na madhara yasitokee kwa wengine, tujitahidi kujitolea sana.”
Crédito: Link de origem