top-news-1350×250-leaderboard-1

Kambaya: Siasa si ushabiki, ni mpango wa maisha

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdul Kambaya, amewataka wananchi kuacha kuangalia siasa kwa jicho la ushabiki na badala yake kuitazama kama njia ya kupanga na kuboresha maisha yao ya kila siku, yakiwemo masuala ya elimu na afya.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Nachingwea, wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Kambaya amesema wazazi wana jukumu kubwa la kufanya maamuzi sahihi ya kisiasa kwa mustakabali wa watoto wao.

“Siasa si ushabiki, bali ni mpango wa maisha. Wazazi mna jukumu la kupiga kura kwa ajili ya maisha bora ya watoto wenu, kwani wao hawana uwezo wa kupiga kura. Maamuzi yenu leo ndiyo yatakayoamua aina ya elimu na huduma za afya watakazopata watoto wenu kesho,” amesema Kambaya.

Aidha, amehimiza wananchi waendelee kuiunga mkono serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na hatua mbalimbali za maendeleo ambazo zimeendelea kuonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kambaya alisisitiza kuwa Watanzania hawapaswi kuchagua vyama kwa misingi ya matumaini yasiyo na uhakika, bali kwa kuzingatia rekodi ya utendaji na dira ya maendeleo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.