top-news-1350×250-leaderboard-1

Mauzo ya umeme yameongezeka kwa asilimia 10

Dar es Salaam. Wakati upotevu wa umeme ukifikia asilimia 14.61 katika mwaka ulioishia 2023/2024, mauzo ya umeme yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Ripoti ya sekta ndogo ya umeme iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Mafuta (Ewura) inaonyesha kuwa upotevu wa umeme huo ni ongezeko kutoka asilimia 14.57 iliyokuwapo katika mwaka 2022/2023.

Licha ya kuwa upotevu huu uko juu ya kiwango kinachotakiwa cha asilimia 12 lakini ni pungufu ukilinganishwa na kiwango kilichokuwapo kwa miaka mitatu mfululizo kutoka asilimia 16.22 mwaka 2018/2019 hadi asilimia 14.64 iliyokuwapo mwaka 2021/2022.

Upotevu wa asilimia 14.61 ya umeme wote iliyokuwapo katika mwaka 2023/2024 ni sawa na Megawati 589.75 ikiwa tutatumia megawati 4,032 ambazo zimetajwa na Mkurugenzi wa Ewura, Dk James Mwainyekule kuwa zinazalishwa hadi sasa.

Ili kukabiliana na upotevu huo wa umeme, Ewura iliiagiza Tanesco Kufanya ujenzi na ukarabati wa miundombinu, kuingiza umeme kutoka kwa nchi jirani kwa ajili ya vituo vilivyokuwa mbali na maeneo ya uzalishaji.

Pia Ewura imeitaka Tanesco kuhakikisha kuwa inafanya kampeni kubwa za uendeshaji dhidi ya wizi wa nishati.

Upotevu huu unashuhudiwa wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa, katika mwaka 2023/2024 wastani wa muda wa ukatikaji umeme ulikuwa dakika 554 (saa 9.23) ikiwa ni chini ya kikomo cha dakika 1,536 huku wastani wa ukatikaji wa umeme ukiwa mara 14 ambao ni chini ya mara 26 ambacho ni kiwango kinachotakiwa.

Wastani wa dakika za ukatikaji umeme zilizokuwapo mwaka 2023/24 ni pungufu ikilinganishwa na dakika 1,536 katika mwaka 2022/2023 na dakika 26,820 zilizokuwapo mwaka uliotangulia.
Mkoa wa Rukwa ndiyo uliokuwa ukiongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha dakika za ukatikaji umeme katika mwaka wa ripoti hii kutolewa ambapo ilikuwa 4,228.3, Tabora dakika 3529.30, Morogoro dakika 2,948.80, Kigoma dakika 2,517.9 na Songwe dakika 2,295.99.

Mikoa mingine yenye wastani wa dakika nyingi za ukatikaji umeme ni Simiyu dakika 2,185.87, Kagera dakika 1,854, Mwanza (1,641.2), Iringa (1,514.37) na Mbeya dakika 1,421.3.
Maeneo ambayo yanaonekana kuwa na nafuu ni Kinondoni Kusini ambayo ilikuwa na dakika 106.23, Kilimanjaro dakika 193.84. Ilala dakika 198.91, Dodoma dakika 210.28, Ruvuma (220.59) na Katavi dakika 409.48.

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (Udom), Dk Lutengano Mwinuka amesema miaka ya nyuma miradi ya umeme ilikuwa mingi ambayo haikuwa inafika mwisho lakini sasa kumekuwa na maboresho yanayofanyika na baadhi ya miradi kuonekana kukamilika kwa wakati.

“Uchakavu wa miundombinu ni moja ya sababu, eneo kama Morogoro kuna bwana kubwa la Kidatu linalozalisha umeme kwa kiasi kikubwa lakini ni miongoni mwa wanaopata shida, miundombinu,” amesema.

Amesema ni vyema kuhakikisha umeme wa uhakika unakuwapo muda wote kwani ni moja ya jambo ambalo huangaliwa na wawekezaji kabla ya kutekeleza miradi yao mbalimbali.

“Gharama za uendeshaji kwa wawekezaji ni jambo ambalo linaangaliwa ikiwemo upatikanaji wa nishati inategemeana na shughuli ambazo mwekezaji anafanya, kuna zile ambazo nishati ni kitu cha lazima ikiwa ni umeme, maji au makaa inakuwa ni kitu cha kwanza kabla kuangaliwa kabla ya chochote,” amesema.
Amesema hali hii inaweza kurekebika ikiwa miradi midogo midogo inayotekelezwa katika mikoa na watu binafsi na mwisho wa siku wanaiuzia serikali umeme huo ikisimamiwa ipasavyo na kukamilika kwa wakati.

Alipokuwa akitoa wasilisho lake jana wakati wa uzinduzi wa ripoti hizi, Dk Mwainyekule hadi mwaka 2023/2024 kulikuwa na ongezeko la takribani asilimia 26 ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme ambapo megawati 2,411 zilifikiwa na hadi sasa kama nchi inao uwezo wa kuzalisha megawati 4,032
Katika kipindi hicho, miundombinu ya kusafirisha umeme iliongezeka kwa asilimia 9 na vituo vya kupoza (substation) umeme vilijengwa vinne na ongezeko la miundombinu ya kusambaza umeme iliongezeka kwa asilimia 15.

“Mwaka 2023 kulikuwa na changamoto ya upatikanaji umeme lakini hadi Februari 2025 tatizo hilo lilifikia ukomo baada ya kuanza kwa uzalishaji umeme katika bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambapo megawati 490 zilipatikana. Kuongezeka kwa uzalishaji umeme sasa suala la upatikanaji wa huduma umeimarika na sasa changamoto iliyokuwapo zamani imeondolewa,” amesema.

Mauzo ya umeme

Hili linashuhudiwa wakati ambao mauzo ya umeme yalifikia Sh2.418 trilioni katika mwaka 2023/24 kutoka Sh2.205 trilioni iliyokuwapo katika mwaka uliotangulia. Ongezeko hili ni asilimia 10 zaidi ikilinganishwa na asilimia 4 lililoshuhudiwa kipindi kilichotangulia.

Mbali na mauzo ya umeme, mapato ya Tanesco kutoka vyanzo vingine yaliongezeka kwa asilimia 63 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 25 kulikoshuhudiwa katika mwaka uliotangulia.
Hii inafanya jumla ya mapato ya Tanesco kukua kwa asilimia 15 wakati ambao asilimia 85 ya mapato yote yalitokana na mauzo ya umeme na kiwango kilichobakia kikitoka maeneo mengine.
 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema ni vyema kuwekeza katika uzalishaji kwa kutumia vyanzo vingine vya umeme vilivyokuwa karibu na makazi ya watu ikiwemo upepo, maji ili usafirishaji wake usiwe mrefu jambo litakalopunguza upotevu kabla ya kufika kwa mteja.

“Hata mkulima, akilima mazao yake anataka kuona thamani ya uwekezaji wake kwa kuhakikisha anapunguza upotevu wa mazao kadri anavyoweza vivyo hivyo lifanyike huku, hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa umeme unaozalishwa haupoteikwa kuwekeza katika miundombinu Zaidi,” amesema Dk Mmari.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.