Mtwara. Wenyeviti wa vyama vikuu vya ushirika vya Tamcu, Mamcu, na Tanecu wamevitaka vyama vya siasa vya upinzani kuacha upotoshaji kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani, wakisema kuwa madai kwamba mfumo huo hauna tija kwa wakulima ni potofu.
Wenyeviti hao wametoa kauli hiyo leo Aprili 6, 2025 mbela ya waandishi wa habari wakisisitiza kwamba vyama vya upinzani vimekuwa vikieneza taarifa zisizo sahihi kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wamesema wakulima wanajua vyema changamoto walizokuwa wakikumbana nazo kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huu na hivyo wanaupokea kwa furaha na matumaini mfumo huo unaowaletea manufaa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Taneco, Karimu Chipola amesema kuwa viongozi wa vyama vikuu vya ushirika hawako tayari kuona upotoshaji unaofanywa na vyama vya upinzani ukiendelea.
“Vyama vya upinzani viache kuwapotosha wakulima kuhusu stakabadhi ghalani. Katika mikutano yao ya kisiasa, baadhi ya vyama vya upinzani vinapotosha uma kwa kusema kuwa mfumo huu hauna faida kwa mkulima,” amesema Chipola.
Chipola amesema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, bei ya mazao ilikuwa ya chini na wakulima walikuwa hawana uhakika wa soko.
“Mbaazi huko nyuma zilikuwa zikifikiwa kwa bei ya Sh200 hadi Sh500 kwa kilo, lakini kwa sasa, kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, bei imepanda hadi kufikia Sh2,000 kwa kilo kwa msimu mmoja. Hata ufuta, tumeweza kuuza kwa bei ya Sh3,399,” amesema Chipola.
Pia, Chipola ameeleza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta manufaa katika kudhibiti uuzaji holela wa mazao na kutoa takwimu sahihi za uzalishaji.
Amesema pia mfumo huo umesaidia kila mwaka uzalishaji kuongezeka na bei kuwa nzuri, jambo ambalo linawanufaisha wakulima.
“Katika sekta ya korosho, kila msimu hali inabadilika na tunazidi kupanda. Msimu uliopita, tulifanikiwa kuuza korosho kwa bei ya Sh4,195 kwa kilo, bei ambayo haijawahi kutokea hapo nyuma.
“Sasa unaposema kuwa mfumo huu haufai, siyo kweli,” amesema Chipola, akisisitiza kuwa vyama vya upinzani vichukue jukumu la kusema watawasaidiaje wakulima, badala ya kueneza migogoro kati ya serikali na wakulima.
Mwenyekiti wa Tamcu, Musa Manjaule amesema kuwa ushirika ni chombo cha kisheria kinachosimamia wakulima kwa hiyari yao.
Amevitaka vyama vya upinzani kuacha kupotosha umma kwa kusema kwamba tozo za wakulima ni nyingi.
Manjaule amefafanua kuwa msimu uliopita tozo ilikuwa Sh456 na mkulima alilipa kiasi kisichozidi Sh100 kwa usafirishaji.
“Tozo hii ilikuwa ni ya usafirishaji na siyo kama wanavyosema kuwa tozo ilifikia Sh1,000. Hapo nyuma, hakuna zao lililouzwa zaidi ya Sh2,000, lakini sasa tunaona ushindani wa bei. Katika mfumo huu, tulikuwa tunaitafuta Sh2,000 kwa tochi,” amesema Manjaule.
Manjaule amesisitiza kuwa wakulima wengi tayari wamejiandikisha kwa lengo la kupata pembejeo na kwamba anatarajia hadi kufikia Aprili 10, 2025, pembejeo zitagawiwa kwa vyama vya ushirika.
“Niwaombe vyama vya siasa watafute namna ya kuomba kura bila kutuingiza sisi vyama vya ushirika, kwani sisi siyo wanasiasa,” amesema Manjaule.
Mwenyekiti wa Mamcu, Alhaji Azam Mfaume ameelezea masikitiko yake kuhusu baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kutumia majukwaa yao kuwapotosha wakulima.
“Nilitarajia vyama vya upinzani wangekuja na mipango ya kuwasaidia wakulima badala ya kuzungumzia mifumo kuwa siyo mizuri.
“Wangejikita kuwasaidia wakulima kulima mashamba yao, lakini wao wamejikita kusema mifumo sio salama, jambo ambalo ni upotoshaji,” amesema Mfaume.
Crédito: Link de origem