Arusha. Hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa Kata ya Muriet, jijini Arusha, baada ya kukutwa miili ya watu watatu waliouawa kwa namna ya kinyama katika matukio mawili tofauti na kutupwa katika maeneo ya wazi.
Tukio la kwanza lilitokea Machi 26, 2025, ambapo miili ya watu wawili, mmoja wa jinsia ya kiume na mwingine wa kike, ilikutwa ikiwa imefukiwa ardhini.
Miili hiyo ilionekana kuwa na majeraha makubwa, huku baadhi ya sehemu za miili hiyo zikiwa zimetiwa alama za kuteswa, ikiwa ni pamoja na kutobolewa macho.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP, Justine Masejo amesema kuwa miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa Mount Meru.
“Miili hiyo tumehifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru ili kutoa fursa kwa watu kwenda kutambua miili hiyo huku upelelezi ukiendelea kubaini wahusika na chanzo cha tukio hilo,” amesema Masejo.
Katika tukio la pili, mwili wa mwanaume mmoja ulipatikana asubuhi Aprili 5, 2025, katika Mtaa wa Eluwany, Kata ya Muriet, ikiwa umeachwa kando ya barabara, katika hali ya kutisha.
Hii imeongeza hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku maswali mengi yakiwa wazi kuhusu chanzo cha mauaji haya.
Hali hii imewaacha wakazi wa Muriet wakiwa na wasiwasi, huku upelelezi ukiendelea kutafuta majibu na kubaini wahusika wa vitendo hivi vikali.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akizungumza kwa njia ya simu jana, Aprili 5, 2025, amesema kuwa miili yote ya watu watatu iliyokutwa katika matukio hayo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa ajili ya utambuzi wa majina yao.
“Hii miili ya watu wawili inaonekana kuwa ni wageni kutoka maeneo mengine kwani wakazi wa eneo hilo, pamoja na watu kutoka sehemu mbalimbali, wamekuwa wakienda mochwari kwa muda wa wiki nzima sasa, lakini bado hawajaweza kutambua miili hii wala kutoa majina ya wahanga. Hata ndugu zao hawajaonekana,” amesema Mkude.
Mkude amesema kuwa hospitali hiyo imepewa muda ili kuhakikisha kwamba mwili mwingine ulio patikana leo utatambulika na ndugu wa marehemu.
“Kama itashindikana kutambuliwa, basi tutafuta kibali cha mamlaka husika kwa ajili ya kuzikwa,” amesema.
Mkude ametoa wito kwa wakazi wa Arusha na maeneo mengine ya nchi ambao wamepoteza ndugu zao kuharakisha kufika Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kutambua miili hiyo.
“Ikiwa muda utakapopita na miili hiyo haijatambuliwa, basi tutaendelea na taratibu za kuizika kwa kuzingatia sheria,” amesema Mkude.
Amesema kuwa hadi sasa hawajafanikiwa kujua chanzo cha mauaji hayo ambayo wameomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina huku akiwataka kuongeza ulinzi katika maeneo yao ili kubaini mchezo huo mchafu unaoendelea.
Matukio yalivyokuwa
Tukio la kwanza limetokea Machi 26, 2025 ambapo miili ya watu wawili ilikutwa imefukiwa katika moja ya mashamba, pembezoni mwa korongo katika Mtaa huo wa Eluwany, uliyoko Kata ya Muriet jijini Arusha.
Shuhuda wa tukio hilo, Abrahamu Mollel amesema kuwa alfajiri ya siku hiyo wakati wanakusanya mabua ya ng’ombe na wenzake wawili waliona sehemu udongo ukiwa umepanda pembezoni mwa shamba lao.
“Niliwaambia wenzangu ile ni kichuguu au nini shambani ndio tukasogea tukashangaa kuona udongo ukiwa juu kama kumechimbwa na kufukiwa kitu, na tulipojaribu kufukua kidogo ndio tukaona mkono wa mtu tukaogopa na kupiga simu kwa viongozi wa mtaa na kata,” amesema.
Amesema kuwa, baada ya viongozi na polisi kufika katika eneo la tukio, walilazimika kuufukua mwili wa mtu mmoja aliyevaa mavazi ya suti za michezo.
Mollel amesema walibaini mwili ulikuwa na majeraha makubwa ya kipigo, huku macho yote mawili yakitobolewa. Mgongo wake pia ulionyesha michirizi ya kuashiria kwamba mtu huyo aliburuzwa kabla ya kufukiwa.
Shuhuda mwingine, Anaeli Marwa, alisema kuwa walipokuwa wanajiandaa kuondoka baada ya kushuhudia tukio la kwanza, walishituka tena kuona mkono wa mtu ukiwa juu, huku mwili ukiwa umefukiwa.
Amesema hali hiyo iliwashangaza na walikimbilia kuwapigia simu tena viongozi wao ambao walirejea eneo la tukio na kuufukua. Walikuta mwili wa mwanamke aliyevaa dera lenye madoa madoa, ukiwa umetupwa kifudifudi.
“Polisi walikuwa tayari wamefika mochwari na kuacha mwili wa kwanza, lakini walilazimika kurudi tena baada ya kugundua mwili mwingine wa mwanamke huyu, ambaye alikutwa mita chache kutoka kwa mwili wa awali,” amefafanua Marwa.
Katika tukio la pili leo, Aprili 5, 2025, mwili wa mwanaume mwingine umekutwa umetupwa pembezoni mwa barabara, karibu na daraja maarufu la ‘Kwa John’.
Mwili huo ulionekana kuwa na majeraha makubwa mgongoni, ikionesha kwamba huenda alikuwa ametendewa uhalifu kabla ya kutupwa katika eneo hilo.
Akizungumza eneo la tukio, Balozi wa mtaa wa Darajani, Pinieli Midukieki, amesema kuwa mwili huo uligunduliwa na msamaria mmoja aliyekuwa anawahi kufanya majukumu yake ya kazi alfajiri.
“Msamaria mwema aliona mwili huo pembezoni mwa barabara na mara moja alimpigia simu kiongozi wa mtaa ili kuletwa viongozi wengine kushuhudia.
“Nilipopigiwa simu, nilimjulisha mwenyekiti wangu ambaye alifanya mawasiliano na polisi. Polisi walifika haraka na kuuchukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi,”amesema Midukieki.
Wakazi wa eneo hilo wamesema kuwa miili yote iliyokutwa mpaka sasa hawajafanikiwa kuwatambua, wala hawajaweza kupata ndugu zao, jambo linaloashiria kuwa wahanga hao si wakazi wa eneo hilo.
“Hapa tunaiomba Serikali kuongeza ulinzi, kwani matukio haya mawili yameleta hofu kubwa sana. Sisi tupo mbali na mji na maeneo yetu mengi ni vichaka, huku nyumba zikiwa zimejaa katika maeneo mbalimbali.
“Wahalifu wameona kuwa hili ni dampo la kutupa miili ya watu wanaowafanyia uhalifu, hasa ukizingatia kuwa mashamba yetu ya mahindi ni makubwa na yenye giza,” alisema mmoja wa wakazi, akieleza wasiwasi wao.
Anna Temba, mkazi mwingine wa eneo hilo, amesema kuwa matukio hayo yameongeza hofu kubwa miongoni mwa wakazi, hasa wanawake wafanyabiashara wa mboga mboga na wanafunzi ambao hutoka alfajiri mapema ili kuwahi majukumu yao.
“Hii ni hatari sana na imetuletea hofu kubwa, hasa kwa wanawake na watoto. Tunaomba Serikali iongoze doria na kuongeza ulinzi hapa kwetu, maana wahalifu wanaweza kutudhuru. Ukiona mtu anatekeleza uhalifu na umejua, basi ni lazima akuue ili kuficha ushahidi,” ameongeza.
Wakazi wamesisitiza kuwa ni muhimu Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia uhalifu huu usiendelee na kuwalinda wananchi wa maeneo hayo.
Crédito: Link de origem