top-news-1350×250-leaderboard-1

Grumeti Reserves yatoa msaada wa madawati

Na Malima Lubasha, Serengeti

Kampuni ya Grumeti Reserves inayoshughulika na uhifadhi wa wanyamapori katika mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, imekabidhi msaada wa madawati 50 kwa Shule ya Msingi Mbirikiri yenye thamani ya sh 3.5 milioni ili kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo.

Ofisa Rasilimali watu wa kampuni hiyo, Martha Baare akiongozana na viongozi wenzake Domina Mgelwa na Daud Sauli (TAWA) walikabidhi madawati hayo katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo hivi karibuni mbele ya uongozi wa Halmashauri ya kijiji akiwepo Mwenyekiti William Mwita na Ofisa Mtendaji Yohana Senteu.

Baare amesema Grumeti Reserves wametoa msaada huo wa madawati kwa shule hiyo ikiwa ni mwendelezo wao kusaidia wadau wa uhifadhi wanyamapori wanaopakana na mapori hayo ikiwa ni mchango wao kutokana na faida kidogo wanayopata kurejesha kwa jamii.

Akizungumza na wanafunzi, walimu, uongozi wa kijiji na baadhi ya wananchi waliokuwepo kushuhudia kupokelewa kwa madawati hayo, amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili nao waweze kufikia mafanikio na baadaye kuwa wahifadhi wazuri wa rasilimali hiyo ya taifa na kusaidia jamii.

“ Naomba ninyi wanafunzi na wazazi wenu na wananchi kwa jumla muendelee kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori kwa vizazi ijavyo ,” amesema Baare.

Naye David Sauli kutoka TAWA, amesema kutokana na uhifadhi huu wa wanyamapori wanosisitiza kila mara kuhimiza uhifadhi endelevu na kupiga vita ujangili.

“ Tumepata msaada wa madawati hayo na mingine itakayokuja ni kutokana na wanyamapori hao ambao tunahimiza kuwalinda na kuwahifadhi, wanafunzi naomba ujumbe huu ufike kwa wazazi kauli mbiu yetu inasema ‘Tulithishwe Tuwarithishe” amesema Sauli.

Aidha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbirikiri, Hamisi Mega ameipongeza kampuni hiyo kwa msaada huo wa madawati kwani umeondoa changamoto ya wanafunzi kukaa chini wakati wa ufundishaji na ujifunzaji .

“ Shule ya Msingi Mbirikiri ina wanafunzi 570 madawati yaliyopo ni 244 na madarasa mane ambayo yanatosha kabisa baada ya kupata msaada huo hivi sasa hakuna mwanafunzi yeyote anayekaa chini hivyo natoa ombi maalum kwa Grumeti Reserves mbali na msaada huu pia wasaidiye kufadhili masomo kwa vijana wanaomaliza elimu ya sekondari,” amesema Mwalimu Mega.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mgaya ameishukuru kampuni hiyo kutoa msaada wa madawati hayo kijijini kwake na kuomba kuendelea kusaidia maendeleo ya shule hiyo na jamii ikiwa pamoja na kusaidia ajira kwa vijana wa kijiji, huku Ofisa Mtendaji wa kijiji, Sentau akisema kuwa uongozi wa kijiji kwa kushirikisha wadau wengine wataendelea kuhifadhi wanyama hao na kuzuia vitendo vya ujangili.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.