top-news-1350×250-leaderboard-1

Dk. Biteko: Ufundi stadi injini pekee ya kuwaondolea watu umasikini

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema jamii inapaswa kuwa na mtazamo mpya na kuangalia ufundi stadi kama nguzo pekee ya kuondokana na umaskini.

Amesema Serikali imetekeleza masuala mbalimbali kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanakuwa na tija kwa jamii kwa lengo la kuziba pengo la ajira na kuongeza kipato cha jamii.

Dk. Biteko ametoa kauli hiyo leo Machi 21,2025 akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini na miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Tafiti zinaonyesha ukiwekeza dola moja kwenye ufundi stadi ni sawa na kupata dola nne, maana yake kama mahali ambapo tunapaswa kuwekeza zaidi ni kwenye ufundi stadi ndiyo maana Serikali imeamua kuweka mkazo mkubwa ili watoto wetu waweze kujitegemea,” amesema Dk. Biteko.

Aidha ameitaka Veta kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yamekuwa tishio katika sekta ya ajira na kuwafundisha vijana wajue namna ya kukabiliana nayo.

Dk. Biteko ameipongeza Veta kwa kazi nzuri wanazofanya na kushauri maadhimisho yaendelee kufanyika kila baada ya miaka kadhaa kama nyenzo ya kujipima na kuona palipo na kasoro ili kuboresha na kuongeza tija katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi.

Amesema pia maazimio yote ya mkutano huo Serikali itayachukua kwa uzito wake.

“Miaka 30 ni safari ndefu najua mmepita milima na mabonde…ukiniambia nitoe tathmini ya mkutano huu maoni yangu ni kwamba umefanikiwa sana, mmeifanya Veta watu waizungumze,” amesema Dk. Biteko.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanaendelea kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Serikali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa vyuo 64 katika ngazi ya wilaya na chuo cha Mkoa wa Songwe.

“Tumeweka msukumo mkubwa wa kujifunza kutoka nchi mbalimbali ili kujenga mahusiano makubwa zaidi kati ya Veta na wadau wengine na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji,” amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Veta, CPA Anthony Kasore, amesema wataweka msingi mkubwa kuhakikisha ubora wa mafunzo unazingatiwa ili vijana wanaokwenda kwenye soko la ajira wawe na uwezo.

Aidha amesema wanatarajia kuwapa ujuzi wananchi 80,000 ili kurasimisha ujuzi wao uweze kutambulika katika soko la ajira.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuhakikisha vyuo vya Veta vinajengwa na kuweza kuwafikia Watanzania wengi, sera ya elimu ya mwaka 2014 na maboresho ya mitaala tutaisimamia ili kuwajenga wanafunzi kuwa na maarifa, ujuzi wa kwenda kufanya shughuli mbalimbali,” amesema CPA Kasore.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.