top-news-1350×250-leaderboard-1

Serikali yawahakikishia watetezi haki za binadamu ulinzi wa kisheria

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi amesema Serikali inatambua mchango wa watetezi wa haki za binadamu na inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha wanapata ulinzi wa kisheria.

Akizungumza katika mafunzo ya wanachama wapya wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Maswi alisema tayari wizara hiyo imepokea Sera ya Mfano ya Watetezi wa Haki za Binadamu iliyotayarishwa na THRDC kwa ajili ya kuiingiza kwenye mfumo rasmi wa serikali.

“Tunaendelea kujadiliana na THRDC kuona uwezekano wa kuridhia sera hii au kuiboresha zaidi, ili hatimaye iwe sera rasmi ya serikali na kuwezesha utungwaji wa sheria maalum ya kuwalinda watetezi wa haki za binadamu,” alisema Maswi.

Alisisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kulinda na kutetea haki za binadamu, ikiwemo kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Aidha alisema Serikali inafanya kazi kwa karibu na mashirika hayo, ikiwa ni sehemu ya sera ya ushirikiano na wadau wa haki za binadamu.

Katibu Mkuu huyo pia aligusia changamoto zinazowakabili watetezi wa haki za binadamu, ikiwemo ukosefu wa sheria mahsusi ya kuwalinda.

Alisema Serikali iko tayari kushirikiana na wadau kupokea mapendekezo ya maboresho ya sheria mbalimbali ili kuendana na uhalisia wa kazi za mashirika yasiyo ya kiserikali.

Maswi alitangaza kuwa Serikali inakusudia kuingiza elimu ya haki za binadamu katika mtaala wa shule na vyuo kama njia ya kupunguza matukio ya ukiukwaji wa haki hizo nchini.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, alisisitiza kuwa kazi ya utetezi wa haki za binadamu si rahisi bali ni kazi ya wito na kujitoa kwa moyo kwani watetezi wa haki za binadamu ni sauti kwa wasio na sauti, ni macho kwa wasio na macho na ni nuru ya haki kweye giza la dhulma.

Kwa upande wake Mratibu kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, aliwasihi wananchama wapya wa mtandao huo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo, kanuni na sheria za nchi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalihusisha mashirika yasiyo ya kiserikali 53 yaliyojiunga na THRDC, yakilenga kuwajengea uwezo wanachama wapya katika kutetea haki za binadamu na kushirikiana na serikali katika kusukuma mbele ajenda hiyo.

Mtandao wa THRDC una wanachama zaidi ya 300 wanaofanya shughuli zao Tanzania Bara na visiwani.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.