Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Katika jitihada za kuhakikisha ubora wa bidhaa unafikia viwango vya kimataifa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kupata ithibati ya umahiri wa kimataifa kwa maabara zake 12, hatua inayohakikisha majibu ya sampuli zake yanaaminika ndani na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo Machi 18, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kupitia maabara hizi za kisasa, tumepima sampuli zaidi ya 118,059 na kufanyia ugezi vifaa 36,808. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa sokoni zinakidhi viwango vya ubora,” alisema Dk. Katunzi.
Ameongeza kuwa TBS imewekeza katika mashine za kisasa, zikiwemo hydrostatic pressure test, yenye uwezo wa kupima mabomba ya maji kuanzia kipenyo cha milimita 12 hadi milimita 800 (inchi 0.5 hadi 32).
Dk. Katunzi pia ameonya kuhusu matumizi holela ya vilevi, akisisitiza kuwa tatizo kubwa si ubora wa bidhaa hizo, bali matumizi yasiyo sahihi.
“Tatizo sio kwamba vilevi vilivyoko sokoni havina ubora, bali ni matumizi yasiyo sahihi. Watu wanakunywa kwa kiwango kisichofaa na bila kuchanganya kama inavyotakiwa. Vijana, tukizidisha matumizi mabaya ya vilevi, tunahatarisha nguvu kazi ya taifa kwa siku zijazo,” aliongeza.

Ametoa wito kwa jamii kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vilevi ili kuhakikisha afya na ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla.
Crédito: Link de origem