Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 50 ya uanzishwaji mafunzo ya ufundi stadi, Chuo cha Taifa cha Usairishaji (NIT) kimesema kimeshiriki kutoa mafunzo yenye ujuzi yanayowafanya watu waweze kuajiriwa au kujiajiri baada ya kumaliza masomo.
Chuo hicho kinatumia sherehe hizo sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) yanayoendelea jijini Dar es Salaam kunadi kazi mbalimbali zilizofanywa na wanafunzi wake ambazo ni kielelezo cha jinsi ambavyo kimeshiriki kutoa mafunzo ya ujuzi.
Kazi zinazonadiwa katika maonesho ni za wahitimu wa Shahada ya Uhandisi Mitambo ambapo kuna mashine ya kusinya siagi na mafuta na ile ya kusambaza mbolea shambani iliyotengenezwa na Omari Chamlongo na kitimwendo kinachojiendesha chenyewe kwa kutumia simu au umeme kilichotengenezwa na Iman Dastani.
Akizungumza leo Machi 18,2025 na waandishi wa habari kwenye banda la chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Mgaya, amesema chuo kina jukumu la kutoa mafunzo kwa Watanzania ambayo yamejikita kutoa wataalam wenye ujuzi.

“Kazi za vijana wetu ambazo wamezileta hapa ni za ujuzi zaidi, katika kuadhimisha miaka 50 ya uanzishwaji wa mafunzo ya ufundi stadi sisi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji tumeonyesha jinsi ambavyo tunashiriki kutoa mafunzo ya ujuzi. Tumeelekezwa taasisi za mafunzo zijikite kutoa ujuzi ambao utamfanya mwanafunzi anapomaliza aweze kuajiriwa au kujiajiri.
“Kazi hizi zimetokana na jitihada za chuo kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata ujuzi zaidi utakaowawezesha kufanya vitu vizuri zaidi,” amesema Dk. Mgaya.
Naye Chamlango aliyebuni mashine ya kusinya siagi na mafuta, amesema aliangalia matatizo yaliyoko kwenye jamii na kuyatafutia majibu kwa kubuni mashine inayofanya kazi mbili kwa wakati mmoja.
“Niliwatazama wajasiriamali wadogo ambao wanatumia mashine mbili kufanya kazi mbili tofauti, nikaja na mashine moja ambayo inafanya kazi mbili kwa wakati moja. Baada ya majaribio imeonyesha matokeo chanya, nawashauri Watanzania kubuni vitu mbalimbali na kuja na mawazo chanya ambayo jamii itaweza kunufaika nayo,” amesema Chamlango.
Naye Dastani aliyetengeneza kitimwendo amesema kinaweza kufanya kazi kupitia simu ya mkononi kukiendesha hasa kwa mtu mwenye ulemavu wa viungo ambaye hawezi kutumia mikono kukiendesha.
“Kiti hiki unachaji kama simu halafu unakitumia, kinaweza kukaa masaa manane hadi tisa kwahiyo mgonjwa au mtu mwenye ulemavu anaweza kujiendesha mwenyewe au akaendeshwa na mtu mwingine kwa kutumia simu yake. Lengo ni kusaidia watu wenye ulemavu na kupunguza utegemezi kwa watu wengine,” amesema Dastani.
Crédito: Link de origem