Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa onyo kali kwa waganga wanaoshiriki vitendo vya kikatili dhidi ya watoto, ikiwamo kukata vimeo, kung’oa meno na kukata ngozi ya chini ya ulimi (udata), kwa madai ya vitendo hivyo ni vya kinyume na sheria na vinakiuka haki za watoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Alex Mkama amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivi, kwa kuwa ni ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
Kamanda Mkama ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na kuepuka kuwapeleka watoto wao kwa waganga wa jadi wanaofanya vitendo hivi, akisisitiza kuwa wazazi watakaoshirikiana na waganga hao watachukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hili linakuja baada ya uzinduzi wa kampeni ya kitaifa inayolenga kukomesha vitendo vya ukeketaji wa viungo vya kinywa kwa watoto.
Kamanda Mkama, amesema Jeshi la Polisi linahusika katika kulinda usalama wa raia na mali zao, na kwamba usalama wa afya za wananchi ni sehemu muhimu ya jukumu hilo.
Akizungumza kuhusu vitendo vya matibabu yasiyo ya kitaalamu yanayohatarisha afya za watoto, Kamanda Mkama amesisitiza kuwa, polisi watachukua hatua kali dhidi ya watu wanaoshiriki vitendo vya ukatili kwa watoto.
Ameeleza kuwa, hospitali zipo na ndiyo sehemu halali ya kutoa huduma za afya, akionya vitendo kama vile kukata vimeo, kung’oa meno kwa madai ya kuwa ya plastiki au kukata ngozi ya chini ya ulimi (udata), ni kinyume na sheria na vinatishia afya za watoto.
“Sisi kama Jeshi la Polisi tunalinda usalama wa raia na mali zao, ukizungumzia usalama ni pamoja na usalama wa afya za watu. Ikiwa kuna watu wanafanya matibabu yasiyokuwa ya kitaalamu na yenye kuleta madhara, hasa kwa watoto, sisi kama jeshi la polisi tutahakikisha tunachukua hatua.
“Hospitali zipo, mtoto akiumwa, apelekwe hospitali apate vipimo na matibabu, siyo kumkata kimeo, kumng’oa meno kwa madai ya kuwa ya plastiki, ama kumkata ngozi ya ulimi,” amesema Kamanda Mkama.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo amesema vitendo vya ukataji vimeo, ung’oa meno yanayodaiwa kuwa ya plastiki na kukata ngozi ya chini ya ulimi vinatafsiriwa kama ukeketaji wa viungo vya kinywa.
Dk Nzobo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kukomesha mila potofu na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Amesema vitendo hivi vimekuwa na madhara kiafya, ikiwa ni pamoja na madhara ya kuvuja kwa damu nyingi, na pindi inapotokea, mtoto anaweza kufariki dunia kutokana na maumivu au maambukizi.
Aliongeza kuwa, kimeo ni kiungo cha kawaida kama viungo vingine vya binadamu, na kwamba kumkataa mtoto kimeo kwa madai ya kukohoa ni uongo.
“Kukohoa ni dalili ya ugonjwa wa kawaida, ambayo inaweza kusababishwa na minyoo au maambukizi mengine, na inatibiwa kwa dawa za hospitali, hususan antibiotics,” alisisitiza Dk Nzobo.
Akizindua kampeni ya kupinga ukeketaji wa viungo vya kinywa kwa watoto, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Besti Magoma amesema kampeni hiyo itahusisha wadau mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini, walimu, vyombo vya ulinzi na usalama, waganga wa jadi, watumishi wa afya na watumishi ngazi ya jamii.
Dk Magoma amesisitiza kuwa utafiti unaonesha kuwa waganga wanaoshiriki vitendo vya kukata watoto vimeo, kuwang’oa meno ni wale ambao hawajasajiliwa kisheria na Baraza la Tiba za Asili.
“Vitendo vya kukata vimeo na kuwang’oa meno kwa watoto ni kinyume na sheria. Waganga hawa hawajasajiliwa, tutatoa elimu kupitia kampeni hii ili kuwasaidia kuelewa madhara ya vitendo hivyo,” amesema Dk Magoma.
Oswad Nyamoga ni mmoja wa wazazi ambaye aliwahi kumpeleka mtoto wa kaka yake kwenda kukata kimeo amesema baada ya mtoto kukatwa kimeo, alitokwa na damu nyingi na baadaye alipata matatizo ya kula, hasa akishindwa kula vyakula vigumu na vya moto.
Naye, Asha Hamis amekiri kumpeleka mjukuu wake kwa mganga kumng’oa meno yanayodaiwa kuwa ya plastiki.
Amesema alifanya hivyo baada ya kupokea ushauri kutoka kwa mganga, lakini alijuta baadaye aliposhuhudia madhara ya kumng’oa meno mtoto huyo.
“Nilimpeleka mjukuu wangu kwa mganga kumng’oa meno aliyozaliwa nayo, lakini baadaye mtoto alikosa meno, na sasa wanamtania kwa sababu ana mapengo. Hata hospitalini waliniambia kuwa meno aliyong’olewa yanaweza yasikue tena au yakaota kwa kuchelewa. Najuta kwa kumpeleka kwa mganga,” amesema Asha.
Crédito: Link de origem