top-news-1350×250-leaderboard-1

Serikali yashangaa CAF kufungia uwanja wa Benjamin Mkapa

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Serikali imeshangazwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) wa kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa, licha ya kufanyiwa marekebisho makubwa na kuwa tayari kwa mashindano ya kimataifa.

CAF ilitoa taarifa ya kufungia uwanja huo kwa madai ya kutokidhi viwango vya ubora, hasa eneo la kuchezea (pitch), na kuitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutuma jina la uwanja mbadala kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba SC na Al Masri, unaotarajiwa kuchezwa Aprili 9, 2025. Tayari TFF imependekeza Uwanja wa Amahoro, Rwanda kama uwanja mbadala.

Akizungumza Machi 12, 2025, jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema wamepokea taarifa ya CAF kwa mshangao mkubwa, kwani marekebisho yaliyohitajika yalishafanyika na uwanja uko tayari.

“Wakaguzi wa CAF walifanya ukaguzi wiki mbili au tatu zilizopita baada ya mechi ya Simba na Azam. Tumewasiliana na TFF na kuwaelekeza wawataarifu CAF waje wakague tena kwa sasa, kwa sababu uwanja umefanyiwa maboresho na upo tayari kwa mechi za kimataifa,” amesema Msigwa.

Serikali imesisitiza kuwa inaendelea kushirikiana na TFF kuhakikisha uwanja huo unabaki kuwa sehemu ya mashindano ya kimataifa na kwamba CAF inapaswa kuja kufanya ukaguzi mpya kabla ya kutekeleza uamuzi wa kuufungia.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.