top-news-1350×250-leaderboard-1

Utafiti wabaini ukata kukwamisha watu kuzaa

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) imeonesha watu wengi wanashindwa kuwa na idadi wanayoitaka ya watoto kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi.

Kwa kutumia utafiti wa kitaaluma ikiwa ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa na UNFPA kwa kushirikiana na YouGov katika nchi 14 zinazowakilisha zaidi ya theluthi moja ya watu duniani, ripoti hiyo imebaini mtu mmoja kati ya watano hatarajii kuwa na idadi ya watoto anayotamani.

Ripoti hiyo iliyotoka Juni 2025 inaonesha asilimia 39 ya waliohojiwa wenye umri wa zaidi ya miaka 50 walisema hawakufanikisha kupata idadi ya watoto waliotamani, huku asilimia 11 wakieleza mzigo usio sawa wa malezi unaweza kuwazuia kupata watoto.

Sababu kuu zilizotajwa kuchangia ni gharama kubwa ya kulea watoto, kutokuwa na uhakika wa ajira, changamoto za makazi, hofu kuhusu hali ya dunia na ukosefu wa mwenza anayefaa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo zaidi ya nusu ya watu walisema masuala ya kiuchumi ni kikwazo kwao kupata idadi ya watoto wanaotamani kuwa nao.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Dk Natalia Kanem amesema tofauti na ilivyokuwa ikiaminika kwamba watu wengi hawako tayari kupata watoto kwa sababu hawataki kuwa wazazi utafiti umeonesha kinachosababisha hali hiyo ni hali ya uchumi.

“Tatizo si kwamba watu hawataki kuwa na watoto wengi, bali ni ukosefu wa chaguo, na hili lina madhara makubwa kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla. Hali hii ni matokeo ya kutokuwa na kipato cha uhakika kuweza kumudu mahitaji ya familia, kukosa msaada wa malezi na hata gharama kubwa za huduma za afya ya uzazi,” amesema Dk Kanen.

Kilichobainika kwenye utafiti huo kinashabihiana na maoni ya baadhi ya vijana waliozungumza na Mwananchi kuhusu matokeo hayo.

Edson Lyimo, mkazi wa Mikocheni jijini Dar es Saaam amekiri kwamba hali ya maisha inamfanya awe makini ili asikutane na changamoto kwenye malezi.

“Kama uchumi wako haujakaa vizuri huwezi kuzaa tu, mimi nimeshapanga watoto wawili wanatosha, hivyo katika mizunguko yangu sina mpango kabisa wa kuongeza watoto maana sitakuwa na uwezo wa kuwahudumia,” amesema Lyimo.

Kwa upande wake, Mwanaisha Ngunde mkazi wa Buza, Dar es Salaam amesema licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa watoto hali ya maisha inamfanya kuwa na ukomo.

“Napenda sana watoto ila mume wangu amesema wasizidi wanne, tunao watatu hapa tukipata mmoja wa mwisho basi, sasa hivi kila kitu kinahitaji pesa ili maisha yaende vizuri hakuna mambo ya kupeleka watoto kwa ndugu hivyo ukizaa uwe tayari kuwahudumia,” amesema Mwanaisha.

Wakati hao wakieleza hivyo, Muhidin Mfupa mkazi wa Mbagala amesema suala la watoto ni mipango ya Mungu hivyo atakuwa tayari kuwapokea kwa idadi atakayojaaliwa.

“Watu wanahangaika kutafuta watoto, halafu mimi nina uwezo wa kuzaa nijizuie, nitawapokea watoto wote ambao Mungu atanijalia kwanza kila mtoto anakuja na riziki yake,” amesema Mfupa.

Ripoti hiyo imekwenda mbele na kuonya dhidi ya hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi katika kukabiliana na viwango vya kuzaliwa vinavyopungua kama vile kutoa motisha za kifedha kwa kupata watoto au kuweka malengo ya uzazi kwa kuwa sera hizo mara nyingi hazifanyi kazi na zinaweza kukiuka haki za binadamu.

Badala yake, shirika hilo linahimiza serikali kuwawezesha watu kufanya maamuzi ya uzazi kwa hiari, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika makazi nafuu, ajira zenye staha, likizo ya uzazi, na huduma kamili za afya ya uzazi pamoja na taarifa sahihi.

Kufuatia hilo UNFPA inazitaka jamii kushughulikia kila namna ya ukosefu wa usawa wa kijinsia unaoathiri maamuzi ya watu kuhusu familia, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa mifumo itakayozuia mwanamke kutopoteza kazi yake akipata ujauzito.

Pendekezo lingine ni kwa nchi kuimarisha mfumo wa huduma za afya ya uzazi na kuhakikisha zinatolewa kwa gharama nafuu.

Pia, imependekezwa kuondolewa kwa fikra potofu kuhusu ushiriki hafifu wa baba wakati wa hatua za awali za malezi ya mtoto hali inayosababisha wanaume kukosa likizo ya uzazi yenye malipo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.