Kyela. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema Serikali imefungua fursa za ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi ya Tanzania na Malawi, kupitia mradi wa ujenzi wa barabara ya Ibanda – Kajunjumele mpaka bandari ya Itungi na Kiwira, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hususan makaa ya mawe.
Waziri Bashungwa amesema hayo jana Oktoba 2, 2023 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Njisi Kata ya Kasumulu kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi, katika ziara ya kikazi; akiongozana na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
“Lengo la Serikali ni kujenga uhusiano baina ya nchi zetu na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa kusafirisha malighafi ya kutengeneza saruji, makaa ya mawe, mazao kama mpunga na kakao na mengine mengi ambayo huzalishwa na wakulima nchini,” amesema.
Amesema kupitia fursa hizo ni vyema sasa wananchi kujikuta katika kuzalishaji mazao yenye tija na ambayo yatapata masoko ya uhakika katika nchi za jirani na kusafirisha kupitia kituo cha pamoja cha forodha baina ya Tanzania na Malawi.
“Tumekuja na Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kukagua utekelezaji wa miradi ya barabara tumeanzia Wilaya ya Rungwe, na tupo hapa Kyela kukagua mradi wa barabara ya Itungi-Kajunjumele mpaka bandari ya Itungi na Kiwira ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami lengo ni kufungua fursa za kiuchumi na mashirikiano baina ya nchi zetu mbili,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa fedha ameagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kuacha kunyanyasa Wafanyabishara kwa kuwafungia maduka na kwamba kitendo hicho kinasababisha kugeukia uingizwaji wa bidhaa magendo nchini.
“Rais anataka viwango vya kodi vishuke, sasa huo mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa kuwafungia maduka wafanyabishara wadogo, ni kuwanyanyasa; hayo sio maagizo ya Serikali sasa, hata hivyo nasisitiza wafanyabishara kulipa kodi kwa hiari,” amesema.
Aidha Waziri Mwigulu amewataka TRA kuweka mfumo mzuri wa ukusanyaji wa mapato utakao iwezesha mamlaka hiyo kujenga uhusiano mzuri na na wafanyabishara kwa lengo la kuwawezesha kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.
Naye mfanyabiashara, Tauli Joel amepongeza hatua hiyo ya Mwigulu kupiga marufuku wafanyabishara wadogo kufungiwa maduka, akidai kuwa hali hiyo inasababisha wengi wao kubadili biashara sambamba na kufungua nchi jirani ya Malawi.
Credit: Source link